ETETA | Home juu

Mhe. Loata Erasto Ole Sanare

Mkuu wa Mkoa Morogoro


Eng. Emmanuel Masasi Kalobelo

Katibu Tawala Mkoa Morogoro

Eng. Joyce Meshack Baravuga

Afisa Elimu Mkoa Morogoro

 • Mkuu wa Mkoa

  Mkuu wa Mkoa Morogoro, Mhe. Loata Erasto Ole Sanare

 • Katibu tawala mkoa

  Katibu Tawala Mkoa Morogoro, Mhandisi. Emmanuel Masasi Kalobelo

 • Picha ya pamoja...Afisa Elimu MKoa, Eng. Joyce Baravuga(katikati) na wadau wengine wa ETETA

 • Prof Kahimba kutoka Sua na Afisa Elimu Mkoa Eng. Baravuga wakiwa katika kikao cha kufanikisha elimu kwa TEHAMA katika mkoa wa Morogoro

 • Shoes slide img

Maana ya ETETA

Maana ya ETETA ni Elimu kwa TEHAMA Tanzania (ETETA). ETETA ni mpango endelevu wa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ulioanza mwaka 2018 katika Mkoa wa Morogoro kwa lengo la kutumia TEHAMA katika idara ya Elimu na kuufanya Mkoa wa Morogoro ifikapo mwaka 2022 kuwa Mkoa wa kidigitali.

Mambo yanayofanywa na ETETA . Kwa kutumia Elimu kwa TEHAMA tunaweza kufanya mambo yafuatayo:-

UFUNDISHAJI NA UJIFUNZAJI

Kuboresha ufundishaji na ujifunzaji kwa kutumia TEHAMA.

UTUNZAJI WA TAKWIMU

Kuimarisha utunzaji wa takwimu kwa kutumia TEHAMA

ZANA ZA KUFUNDISHIA

Kuandaa maudhui ya masomo na zana za kufundishia kwa kutumia TEHAMA e-Content.

UPATIKANAJI WA HABARI

Kuharakisha Upatikanaji wa Habari na taarifa kwa kutumia TEHAMA.

KUTOA MAFUNZO YA TEHAMA

Kutoa mafunzo ya somo la TEHAMA na Matumizi ya Vifaa vya TEHAMA kwa Walimu na Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari

Habari Mpya

Imewekwa 2020-09-26

WALIMU MOROGORO TUTAMPATA NANI TENA KAMA ‘ADSI’?

(Pichani ni walimu, wakufunzi wa vyuo na viongozi mbalimbali wa elimu walioshiriki  mafunzo ya Elimu kwa TEHAMA yaliyotolewa na ADSI hapa Mkoani Morogoro hivi karibuni)

“Huenda warsha ya leo ikawa ya mwisho nikiwa kama mratibu wa mafunzo ya TEHAMA yanayotolewa na ADSI hapa Morogoro”. Hii nii kauli iliyotolewa mwishoni mwa juma lililopita na Mratibu wa mradi wa ADSI Morogoro ndugu Ramadhan Matimbwa. Kwa muda wa wiki nzima, kauli hii imekuwa ikinifikirisha sana juu ya mchango mkubwa usiotarajiwa uliotolewa na ADSI kwa walimu wa Morogoro kwa miaka mitatu mfululizo.

ADSI ni kifupisho cha neno ‘African Digital Schools initiative’. Ni mradi usio wa serikali uliolenga kuleta mageuzi katika shule zetu za Afrika kwa kuzifanya kuwa za kidijitali ili kuendana na mahitaji ya dunia ya sasa. Mradi huu umekuwa ukitekelezwa katika nchi tatu za Afrika ikiwemo Kenya, Tanzania na Cote d’voire. Kwa hapa kwetu Tanzania, ni mikoa miwili pekee iliyobahatika kufikiwa na mradi huo ambayo ni Morogoro na Pwani.

Katika kutekeleza mradi huo, ADSI waligawa vifaa vya TEHAMA mashuleni ikiwemo Kompyuta na ‘Tablets’ kwaajili ya kufundishia na kujifunzia. Walisajiliwa walimu wanaofundisha masomo ya Sayansi, Hisabati na Lugha (STEM) kwaajili ya kupewa mafunzo ya matumizi ya TEHAMA katika ufundishaji wao kwa muda wa miaka mitatu tangu mwaka 2017.  Viongozi wa elimu wakiwemo wakuu wa shule, waratibu elimu, maafisa mbalimbali na wakufunzi wa vyuo vya ualimu nao hawakuachwa nyuma katika mafunzo hayo.  

Mazoezi kwa vitendo yalikuwa ya kutosha kiasi ambacho kwa mwalimu mzembe mzembe asingeweza kuendelea na mafunzo hayo kwa miaka yote mitatu. Wanastahili pongezi nyingi sana walifanikiwa kudumu katika mafunzo hayo hadi mradi unapoelekea mwishoni.

Ukitafakari manufaa ya mradi huu hapa kwetu Morogoro utagundua mambo makubwa yaliyofanyika ambayo ni lazima yabaki kwenye kumbukumbu za kila mmoja wetu.

Kwanza, tunafahamu kwamba walimu wengi wa msingi na sekondari waliosoma miaka ya nyuma hakukuwa na somo la TEHAMA mashuleni wala katika vyuo vya ualimu. Ni sawa na kusema kuwa, tulikuwa na walimu wasio na ujuzi wa TEHAMA katika wakati ambapo kila mwanafunzi anahitaji kufundishwa ujuzi huo.  Itakumbukwa kuwa hapo nyuma miaka ya 2000, serikali ilijaribu kuweka somo linalojitegemea la TEHAMA kwa shule za msingi, lakini mitaala mipya ya 2015 ililiondoa somo hilo na kuunganisha maudhui hayo katika somo la Sayansi kuanzia Darasa la tano. Unaweza kutafakari maana ya mabadiliko hayo ukajijibu mwenyewe.

Pili, ADSI imeleta kitu kipya (value added) kwa walimu kukutana na kujifunza TEHAMA kwa miaka mitatu mfululizo tofauti na mafunzo ya masomo yaliyozoeleka kwa walimu. Ilikuwa ni jambo la pekee sana ukifika shuleni unawakuta walimu wamekaa kikundi na kompyuta zao wakijadili na kufanya majaribio mbalimbali ya TEHAMA yanayotolewa na ADSI kwa njia ya mtandao na nje ya mtandao. Binafsi hii ilikuwa inanikumbusha shughuli niliyowahi kupitia kwenye vimbweta vya chini ya mti wa ‘mdegree’ pale chuo kikuu cha Dar es Salaam.  Kwakuwa shahada nyingi husomewa kwa muda wa miaka mitatu, ni sawa na kusema kuwa ADSI wametuongezea shahada nyingine ya TEHAMA kwa walimu wa Morogoro na Pwani.   

Tatu, Mafunzo ya ADSI yameisaidia sana serikali ya Tanzania ambayo ndiyo hasa yenye jukumu la kutoa mafunzo kazini kuimarisha watumishi wake wakiwemo walimu. Kwa kuwalea walimu kiTEHAMA kwa miaka yote mitatu, ni wema usiopimika ambao pia umeipunguzia mzigo serikali yetu. Inawezekana kabisa kwamba katika miaka yote hiyo mitatu, baadhi ya walimu hawakuwahi kushiriki mafunzo mengine yoyote kazini (Inservice training) isipokuwa ya TEHAMA tu chini ya ADSI.

Mfano, katika shule ninayofundisha tuliwahi kutembelewa na wathibiti ubora wa shule kanda ya mashariki wiki chache zilizopita. Wakati wa majumuisho ya ukaguzi wao uliodumu kwa siku mbili, nililazimika kuuliza swali lililotanguliwa na maelezo kama ifuatavyo;

“Nimeona mjadala wetu tangu mwanzo hadi mwisho tumezungumzia masuala yahusuyo mbinu za ufundishaji ikiwemo andalio la somo na mpango kazi (Pedagogical issues), lakini tukiwa vyuoni huwa tunafundishwa ualimu katika pande kuu mbili ambazo ni mbinu za ufundishaji na somo la kufundishia (Pedagogy + Teaching subject). Lakini pia, nina takribani miaka saba kazini sijawahi kukutana na mafunzo yoyote juu ya somo langu la kufundishia (Biology). Sana sana nimehudhuria mafunzo ya kutosha ya TEHAMA ikiwemo ya ADSI kiasi cha kujiuza swali, kwani mimi nimekuwa mwalimu wa TEHAMA?’’.

Baada ya maelezo hayo nikauliza swali; Kwakuwa miaka ya hivi karibuni upande wa somo la kufundishia (Teaching subject) haupewi kipaumbele kwenye ukaguzi na hata kwenye mafunzo kazini, nyie kama wakaguzi mmeshajiridhisha kwamba hakuna tatizo tena katika upande huo kwa walimu? Nafikiri wapo walimu wengine pia wanaoweza kujiuliza swali kama hilo baada ya kushirki mchakamchaka wa ADSI hapa Morogoro.

Nne, ADSI imesaidia sana kuunganisha walimu na viongozi wa shule za Morogoro na kuwa kitu kimoja. Hawa wote wanakutana katika darasa moja mara kwa mara na kujifunza pamoja. Kwa lugha ya kisasa tunasema wamekuwa ma-‘Class mates’ kwakuwa wamehesabu miaka mitatu pamoja darasani.

Moja ya kazi walizotakiwa kufanya katika mradi huu ni kuingia kujibu au kujadili maswali mtandaoni ambapo mratibu wa Mradi ndugu Matimbwa anauliza swali la TEHAMA na kila mmoja anatoa mtazamo wake. Hii ilikuwa inaitwa Chart and Discussion.  Kila mmoja aliweza kusoma kilichoandikwa na mwenzake na walikuwa wanaonana kwa picha mtandaoni. Wakati mwingine waliendesha mijadala na mfunzo kwa nijia ya video. Hii imewaunganisha wanataaluma hao na kubadilishana ujuzi.

Ni vigumu kueleza mazuri yote yaliyofanyika kwa miaka mitatu ndani ya makala moja kama hii. Lakini itoshe kusema kuwa, ADSI imegusa sana akili na mioyo ya walimu, viongozi na wadau wengine wa elimu. Kuna walimu walikuwa waogopa wa teknolojia lakini sasa ni watumiaji wazuri wa teknolojia. Ujuzi tulioupata hautufai darasani pekee, bali katika maisha yetu yote ndani na nje ya shule. ADSI imetufanya kuwa walimu wa kisasa na kutuongezea hadhi mbele ya wanafunzi wetu. Ndiyo maana kauli ya ndugu Ramadhani Matimbwa ya kuashiria mwisho wa mradi, imeacha swali kubwa kwa walimu wengi Morogoro kuwa, tutampata nani tena kama ADSI?

Imeandaliwa na;

Mwl. Wilson Anatory

Kilakala Sekondari - Morogoro   

Soma Zaidi

Mbinu za Kukuza Ufaulu katika Mkoa wa Morogoro

Mbinu za Kukuza Ufaulu

Katika Kukuza kiwango cha ufaulu katika Mkoa wa Morogoro, Idara ya Elimu Mkoa wa Morogoro imeunda mbinu ijulikanayo kama C4 K4 ili kukuza kiwango cha ufaulu katika Mkoa wa Morogoro.

Soma Zaidi

Wahisani

 • Wahisani
 • Wahisani
 • Wahisani
 • Wahisani
 • Wahisani