ETETA | Home juu

Mchapisho ya Habari za Nanenane

Kilimo
Kilimo bora cha Bustani Kilimo bora cha Chainizi Kabichi Kilimo bora cha Kunde
Kilimo bora cha Kunde Kilimo bora cha Mchicha Kilimo bora cha Mhogo
Kilimo bora cha Mnavu Kilimo bora cha mpunga Kilimo bora cha Sukuma wiki
Kilimo cha Mboga mjini Mfuko wa pembejeo
USINDIKAJI WA MUHOGO
Uvuvi
association representing the interest of various stakeholders athari za uvuvi haramu faidika na chakula bora kwa gharama nafuu cha samaki
kujenga mazingira wezeshi mafanikio katika sekta ya uvuvi mbinu bora za ufugaji samaki aina ya perege
ufungaji nwa samaki aina ya mwatiko uhifadhi wa samaki kwa kutumia barafu uhifadhi wa samaki kwa kutumia barafu
Mifugo
chakula bora cxhja mifugo malisho bora ya mifungo na jinsi nya kuyaendeleza utengenezaji wa vyakula bora vya mifugo
uzalishaji wa mbegu bora au vipando vya malisho
Ufugaji wa kuku
kupe na athari zake kwa mifugo mdondo ni hatari kwa kuku minyoo ya kuku
ufugaji wa kuku wa kienyeji -ifakara ufungaji bora wa kuku wa kienyeji ugonjwa wa kuharisha damu
ugonjwa wa mdondo utunzaji bora wa vifaranga
Taasisi za Elimu zinazojihusisha na kilimo
SUA-centre for information & communication technology AGROECOLOGY HUB IN TANZANIA-SUA College of Forestry, Wildlife and tourism (Department of Wildli
COLLEGE OF SOCIAL SCIENCES AND HUMANITIES(CSSH) jordan university college of st.Augustine Maabara ya kisasa ya udongo
RESEARCH,COMMUNITY&ORGANIZATIONAL DEVELOPMENT ASSOCIATES (RECOD stashahada ya usimamizi wa nyanda za malisho na udhibiti wa ndo Wakala wa vyuo vya mafunzo ya mifugo(LITA)
Ufugaji wa Mbwa
Fahamu ugonjwa wa kichaa cha mbwa kichaa cha mbwa

Habari na Matukio

Prof Adolf Mkenda katibu mkuu wizara ya mali asili na utalii
Bernadeta Kadala, meneja msaidizi wakala wa misitu kanda ya mashariki
Apaikunda mngule meneja mhifadhi kanda ya mashariki


Imewekwa Tarehe 2020-08-09

MANISPAA YA MOROGORO YAZIPIGA 3 BILA HALMASHAURI ZA MIKOA MINNE YA KANDA YA MASHARIKI MAONESHO YA NANENANE 2020

Inawezekana wenzetu wanatamani tushangilie kimyakimya ili isijulikane kama tumewashinda, lakini watusamehe kwakuwa tunashindwa kuficha hisia zetu. Ungekuwa ushindi wa kawaida tungepunguza sauti, lakini kwa ushindi huu wa tatu bila; Morogoro piga Keleleeeeee!!!  

Siku ya jana tarehe 8 Agosti 2020 maarufu kama siku ya nanenane ilikuwa njema kwetu wana Morogoro baada ya halmashauri yetu ya manispaa ya Morogoro kuibuka mshindi wa kwanza katika vipengele vyote vitatu wakati wa kilele cha maonesho ya nanenane yaliyokuwa yakifanyika mkoani Morogoro.  Halimashauri ya Manispaa ya Morogoro imejitwalia jumla ya tuzo tatu baada ya kuzishinda halmashauri, manispaa na majiji yaliyopo katika  mikoa minne ya kanda ya mashariki ikiwemo Morogoro, Pwani, Dar es Salaam na Tanga.

Manispaa ya Morogoro ambayo ndiyo mwenyeji wa maonesho hayo, imekuwa mshindi wa kwanza katika vipengele vifuatavyo; (1) Kundi la Manispaa na Majiji yote ya mikoa minne, (2) Mshindi katika Halmashauri za mkoa wa Morogoro na (3) Mshindi katika maonesho ya kikanda (Kanda ya mashariki).  

Tuzo hizo zilitolewa na Waziri wa Afya maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto Mhe. Ummy Mwalimu ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi katika kilele cha maonesho ya nanenane kanda ya mashariki.

Dalili za ushindi huo zilionekana tangu mwanzo wa maonesho hayo ambapo Manispaa ya Morogoro ilikuwa imejipanga kikamilifu kuhakikisha inakuwa mshindi. Wakati maonesho yalipoanza, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Bakari Msulwa alitembelea mabanda ya halimashauri ya Manispaa Morogoro ambapo alisistiza mambo makuu mawili. “Kazi zetu kuu ni mbili katika maonesho haya; kwanza ni kuhakikisha ushindi unabaki nyumbani kwetu, pili ni kuhakikisha haya mambo mazuri tunayoyaonesha yanafanyika kivitendo huko kwa wakulima na siyo kuishia hapa kwenye viwanja vya maonesho tu”. Alisema Mhe. Msulwa.   

Bila shaka, ushindi huu mkubwa umekata kiu hiyo aliyokuwa nayo Mkuu wa wilaya ya Morogoro pamoja na viongozi wote waliohusika kuratibu na kusimamia maonesho hayo. Ushindi huo unaongeza chachu kwa wakulima wa halmashauri ya Manispaa ya Morogoro na hata wale wa wilaya zingine za Mkoa wa Morogoro ikizingatiwa kuwa mkoa huo ni ghala la taifa la chakula.  

Maonesho ya nanenane ya mwaka huu yaliongozwa na kaulimbiu isemayo; “Kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Chagua Viongozi bora 2020”. Kumalizika kwa maonesho hayo ni mwanzo wa kujiandaa na maonesho mengine ya nanenane kwa mwaka ujao 2021. Manispaa ya Morogoro ndiyo sisi, tatu bila zingine zinakuja!

Imeandaliwa na; Wilson Anatory

ETETA TV - MOROGORO   

Soma Zaidi
Imewekwa Tarehe 2020-08-07

AFISA ELIMU MKOA WA MOROGORO ATEMBELEA MAONESHO YA NANENANE, ATOA ZAWADI KWA WATUMISHI WA IDARA YA ELIMU MANISPAA YA MOROGORO

(Pichani ni Afisa Elimu Mkoa wa Morogoro Eng. Joyce Baravuga (wa pili kutoka kulia) akiwa na watumishi wa Idara ya Elimu Msingi na Sekondari Manispaa ya Morogoro katika maonesho ya nanenane yanayoendelea mkoani Morogoro)

Inawezekana wewe si mwanafunzi lakini unasomesha watoto. Hii ina maana kwamba  kila mtu anahusika na suala la elimu kwa namna moja au nyingine. Mwalimu makini hupenda kukagua kazi na maendeleo ya wanafunzi wake kila mara ili kuboresha mbinu za ufundishaji wake. Hiki ndicho alichokifanya Afisa Elimu Mkoa wa Morogoro Eg. Joyce Baravuga kiongozi na mwalimu namba moja mkoani Morogoro.

Mapema leo tarehe 7 agosti 2020, kiongozi huyo alitembelea maonesho ya wakulima na wafugaji maarufu kama nanenane.  Kwa kuzingatia kuwa kila mkulima na mfugaji alipita kwenye mikono ya mwalimu kabla ya kujiingiza kwenye ajira hiyo, Eng. Baravuga ametembelea maonesho kama mwalimu anayekagua matunda ya kazi yake. Ilikuwa ni ya muhimu sana kwake kufanya hivyo kwakuwa ndiye mwenye sauti ya kushauri maboresho yanayohitajika katika kuandaa wahitimu walio bora kulingana na mahitaji ya nchi. Katika hili, anastahili pongezi kwa kutimiza wajibu wake.

Baada ya kutembelea na kujifunza katika vipando na mabanda mbalimbali ya maonesho, aliwasili katika banda la Idara ya Elimu Manispaa ya Morogoro ambapo alifanya kitu kitakachobaki kwenye kumbukumbu za watumishi wa idara hiyo waliokuwa wakihudumu hapo.  

Mara baada ya kuwasili aliomba kupewa maelezo kama mteja mwingine wa kawaida. Wahudumu waliokuwa wakionesha kujiamini, walieleza kwa umahili mkubwa na kujibu maswali yote yaliyoulizwa na kiongozi huyo. Walimshirikisha kucheza michezo mbalimbali ya chemsha bongo inayotumika kufundishia watoto shuleni na kila mmoja alifurahi sana.  

Eng. Baravuga alionesha kuridhika na maonesho hayo, akaamua kuwapongeza na kutoa zawadi kwa wahudumu wote 15 waliokuwepo hapo kutokana na kuiwakilisha vyema idara ya Elimu Msingi na Sekondari  katika maonesho hayo.  

Nao wahudumu walifurahi sana kwa namna kiongozi wao alivyoridhika na kazi yao hadi kuwazawadia. Waliamua kupiga naye picha ya pamoja kwaajili ya kumbukumbu, huku kila mmoja akipambana kupata picha binafsi ya kumbukumbu akiwa na kiongozi huyo.

Ikumbukwe kuwa, moja ya vitu vilivyokuwa vikioneshwa hapo ni video zilizorekodiwa za masomo ya shule za msingi na sekondari kwa usimamizi wa Idara hiyo. Video hizo ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya ‘Elimu kwa Tehama Tanzania (ETETA) iliyoasisiwa na Eng. Baravuga kama Afisa Elimu Mkoa wa Morogoro tangu mwaka 2018.

Hii ni sera inayolenga kuufanya mkoa wa Morogoro kuwa wa kidijitali ifikapo mwaka 2022 kwa kuongeza matumizi ya Tehama katika taasisi za elimu na nyinginezo.  Video hizo za masomo zinaweza kupatikana katika mtandao wa youtube channel ya ETETA TV inayopatikana ukiwa mahali popote pale ndani au nje ya nchi. Katika maonesho hayo, video hizo zinatolewa bure kwa wananchi wanaofika hapo wakiwa na ‘flash disk’ za kuhifadhia.

Maonesho hayo ya kanda ya mashariki yanahusisha mikoa ya Morogoro, Pwani, Dar es Salaam na Tanga yakiwa na kaulimbiu isemayo kuwa; “Kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi chagua Viongozi bora 2020.

Imeandaliwa na; Wilson Anatory

ETETA TV - MOROGORO

Soma Zaidi
Imewekwa Tarehe 2020-08-05

AFISA ELIMU MOROGORO AFANYA MAKUBWA KWA WANAFUNZI KILAKALA SEKONDARI WALIPOTEMBELEA IDARA YA ELIMU MAONESHO YA NANENANE

(Pichani ni Afisa Elimu Sekondari Manispaa ya Morogoro Dkt. Janeth Balongo (Kushoto) akicheza mchezo wa Chemshabongo na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kilakala Walipotembelea Idara ya Elimu katika maonesho ya nane nane mkoani Morogoro)

Moja ya shule zilizojizolea umaarufu mkoani Morogoro na Tanzania nzima ni shule ya sekondari Kilakala iliyopo katika halmashauri ya manispaa ya Morogoro.  Hii ni shule ya serikali maalumu kwa watoto wenye ufaulu mkubwa. Kwa kifupi ni shule ya wanafunzi wenye vipaji maalumu.

Leo tarehe 5 agosti 2020, wanafunzi hao wa shule ya sekondari Kilakala waliweza kutembelea banda la Idara ya Elimu halmashauri ya Manispaa Morogoro inayoshiriki katika maonesho ya nanenane yanayoendelea mkoani Morogoro. Tofauti na wanafunzi wengi tuliowazoea, wanafunzi wengi wa Kilakala sekondari walionekana kuwa na daftari ndogo (note book) kwaajili ya kuandika kile walichokuwa wakijifunza kwenye mabanda tofauti tofauti ya maonesho. Hii ndiyo namna halisi ya kujifunza, hongereni sana walimu Kilakala sekondari kwa kuwalea hivyo watoto wetu.

Sina hakika kama inatokana na umaalumu wa shule yao, lakini wanafunzi hao walibahatika kumkuta Afisa Elimu sekondari Manispaa ya Morogoro Dkt. Janeth Balongo naye akiwa amekuja kukagua maendeleo ya maonesho katika banda hilo. Kitu kikubwa alichokifanya Afisa huyo, aliamua kuacha mambo yake yote na kushirikiana na walimu wengine walioandaliwa kufafanua mambo mbalimbali yanayofanywa na Idara ya Elimu manispaa ya Morogoro.

Pamoja na mambo mengine, Dkt. Balongo alishiriki kucheza michezo ya chemsha bongo pamoja na wanafunzi hao. Wanafunzi walifurahi sana kwa mapokezi na ukarimu walioupata katika banda hilo ambalo ndilo linalosimamia mustakabali wa masomo yao shuleni.   

Jambo hili liliwakonga nyoyo hata walimu waliokuwa wameambatana na wanafunzi hao kwa kumwona kiongozi huyo akichukua nafasi ya kufundisha wanafunzi kazi ambayo imezoeleka kufanywa na walimu. “Naona wanafunzi wetu wamepata bahati ya kujifunza moja kwa moja kutoka kwa Afisa Elimu” alisema Mwalimu Abel Mkangwa. Naye Mwalimu Patrick Mwaijonga alisema kuwa, “Banda hili tutaendelea kuwa wageni wenu kwa siku tatu mfululizo. Kutokana na wingi wa wanafunzi tumeamua kuwagawa katika makundi matatu, kesho tutakuja hapa na kundi jingine”.

Banda la Idara ya Elimu (Msingi na Sekondari) linapatikana katika jengo la maonesho la halmashauri ya manispaa ya Morogoro. Maonesho ya nanenane kanda ya mashariki yanahusisha mikoa ya Morogoro, Pwani, Dar es Salaam na Tanga yakiwa na kauli mbiu; “Kwa maendeleo ya kilimo, mifugo na uvuvi chagua viongozi bora 2020.

Imeandaliwa na;

Wilson Anatory

ETETA TV - MOROGORO

Soma Zaidi
Imewekwa Tarehe 2020-08-04

IDARA YA ELIMU MANISPAA YA MOROGORO YAWA KIVUTIO MAONESHO YA NANENANE 2020

Pichani ni N/Waziri wa Viwanda na Biashara Eng. Stella Manyanya (Wa pili kutoka kulia); anayefuata kulia kwake ni Mwenyeji wake Mkurugezi wa Manispaa ya Morogoro Mhe. Sheilla Lukuba wakisikiliza maelezo toka Idara ya Elimu Msingi na Sekondari.

Wao wanajiita kiwanda cha kutengeneza rasilimali watu ya nchi, hawa ni Idara ya Elimu Msingi na Sekondari Manispaa ya Morogoro. Wanaendelea kujinadi kuwa, bila wao hakutakuwa na maonesho ya nanenane kwasababu ndiyo wanaotengeneza wahitimu mahili katika fani mbambali ikiwemo wakulima na wafugaji wanaosherehekewa kupitia maonesho hayo. Mimi ni nani hadi niwabishie sasa?

Banda lao linalopatikana katika viwanja vya nanenane jengo la halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, limesheheni zana mbalimbali zinazotumika katika ufundishaji wao. Zana hizi zinabuniwa na kutengenezwa katika vituo vya walimu (Teachers’ Resource Center) na kusambazwa shuleni kwaajili ya kumrahisishia kazi mwalimu. Ukifika pale unaweza ukataka kuuziwa mfano wa kompyuta ukidhani ni  kompyuta halisi. 

Vilevile, wanatoa elimu juu ya mifumo ya kusajili au kuhamisha  mwanafunzi kutoka shule moja kwenda shule nyingine katika mkoa wowote Tanzania kwa njia ya mtandao bila kusafiri. Hii ni mifumo ya ‘Prem’ kwa shule za msingi  na ‘Prems’ kwa shule za sekondari,  inayomsaidia mzazi au mlezi kuokoa rasilimali muda na pesa za safari na hivyo kujiingiza katika shughuli zingine za uzalishaji ikiwemo kilimo.

Kitu cha pekee sana  katika idara hii, utakutana na ETETA TV (Elimu kwa Tehama Tanzania Televisheni). Kama Idara wameamua kutafsiri mitaala ya shule za msingi na sekondari inayotambuliwa na Taasisi ya Elimu Tanzania kutoka katika vitabu kwenda katika video.  Kwa kutumia walimu mahili, Mada za masomo ya msingi na sekondari zimerekodiwa katika video na kuwekwa katika mtandao wa youtube channel ya ETETA TV.  Hii ni hatua muhimu sana hasa pale inapojitokeza changamoto ya upungufu wa walimu.

Hapo mwanafunzi au mtu yeyote anaweza kujifunza akiwa popote Tanzania  au hata nje ya nchi kupitia simu yake au Kompyuta. Watu wenye ‘Flash disk’ wanaofika kwenye banda hilo la Idara ya Elimu Msingi na Sekondari Manispaa ya Morogoro wamekuwa wakipatiwa video hizo bila gharama yoyote.

Mmoja wa wahudumu katika idara hiyo alieleza kuwa, video hizo ziliweza kuwa msaada sana hasa wakati ule wa likizo ya COVID-19 ambapo wanafunzi waliendelea kujisomea kwa njia ya mtandao wakiwa nyumbani.

Linapokuja suala la watahiniwa binafsi (Private candidates), video hizo zitaendelea kuwa msaada kwao na kuwasaidia kujifunza kwa muda wowote wanaohitaji bila. 

Ikumbukwe kuwa ETETA TV, imekuja kama sehemu ya utekelezaji wa sera ya elimu kwa Tehama inayotekelezwa mkoani Morogoro tangu mwaka 2018. Kuifahamu zaidi sera hiyo, tembelea tovuti www.eteta.ac.tz . Ukweli ni kwamba, ubunifu huu hautainufaisha Morogoro pekee bali nchi nzima ya Tanzania.

Maonesho ya nanenane kanda ya mashariki yanaendelea Mkoani Morogoro yakihusisha mikoa minne ya Morogoro, Pwani, Dar es Salaam na Tanga. Kauli mbiu ya mwaka huu ni kuwa; “Kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Chagua viongozi bora 2020”.

Imeandaliwa na; Wilson Anatory

ETETA TV - MOROGORO

Soma Zaidi
Imewekwa Tarehe 2020-08-02

WAZIRI KABUDI AZINDUA MAONESHO YA NANENANE MKOANI MOROGORO

Ni maonesho ya 27 ya wakulima na wafugaji  maarufu kama Nanenane yaliyozinduliwa tarehe 1 agosti 2020 na mgeni rasmi Waziri wa Mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa Prof. Paramagamba Kabudi. Maonesho hayo ya kanda ya mashariki yameshirikisha mikoa minne ikiwemo Morogoro, Pwani, Dar es Salaam na Tanga.

Baada ya kutembelea mabanda ya maonesho na kujionea mbinu na faida mbalimbali zitokanazo na shughuli za kilimo na ufugaji Prof. Kabudi ametoa wito kwa wananchi kujenga tabia ya kutembelea maonesho ya Nanenane ili kupata elimu mpya ya kilimo, ufugaji na uvuvi.

Akimshukuru Mungu kwa kutuepusha na janga la Corona, ameonesha kutambua thamani ya mimea tiba ambayo wananchi wengi wamekuwa wakiitumia kama tiba asili ya kujikinga na virusi vya Corona (COVID-19). Amesisitiza wananchi kutoisahau mimea tiba wanapopanda mazao mengine ya chakula. “Niwahakikishe kuwa, ndani ya miaka mitano ijayo, miti dawa na mimea dawa itakuwa biashara kubwa, sio tanzania tu bali duniani kote” Alisema Prof. Kabudi.

Aidha ameikumbusha mikoa yote ya kanda ya mashariki jukumu kubwa walilonalo la kuhakikisha Tanzania inapaa kiuchumi kutokana na shughuli za kilimo katika maeneo hayo. Akirejea nia ya Hayati Mwalimu Nyererea lipoamua kujenga viwanda vingi mkoani Morogoro alieleza kuwa, Morogoro ni mkoa wenye ardhi na hali ya hewa nzuri inayowezesha kilimo cha mazao ya aina karibia zote na kilimo hufanyika kwa zaidi ya msimu mmoja kwa mwaka.

Pia, Morogoro ni mkoa uliokuwa na nishati ya umeme wa kutosha kutokana na mabwawa makubwa ya kuzalishia umeme yaliyokuwepo.  Umeme huo ndiyo uliokuwa ukitegemewa kuendeshea viwanda vilivyojengwa kwaajili ya usindikaji wa mazao. Zaidi ni kuwa, Mkoa wa Morogoro uko karibu na bandari mbili kubwa za Dar es Salaam na Tanga kwaajili ya kusafirisha mazao ya kilimo kwenda nchi za nje na hivyo kurahisisha biashara.

Kwa msingi huo, Prof. Kabudi amewakumbusha viongozi na wananchi wa mikoa yote ya mashariki kutambua kuwa bado wanalo jukumu hilo la kuhakikisha kuwa wanakuwa kiungo muhimu katika kuipaisha nchi yetu kiuchumi. “Morogoro na kanda ya mashariki ndiyo injini yenye jukumu kubwa la kuifanya nchi yetu ipae kiuchumi” Alisema Prof. Kabudi.

Amesisitiza matumizi ya njia bora za kilimo kuanzia kwenye ulimaji, uvunaji, utunzaji na usindikaji wa mazo ya kilimo. Hii ni pamoja na kuongeza ubora na thamani ya mazao ili wakulima waweze kunufaika vyema na kazi zao za kilimo, uvuvi na ufugaji.  

Katika hatua nyingine, Prof Kabudi ameahidi kupeleka ombi lililotolewa la maonesho ya Kanda ya mashariki kuwa ya kitaifa hapo mwakani 2021. Amewashukuru na kuwapongeza sana wakuu wa mikoa yote ya Morogoro, Pwani, Dar es Salaam na Tanga kwa kusimamia vyema maandalizi yote ya maonesho hayo ya kanda ya mashariki mwaka 2020. Pia amewapongeza makatibu tawala wa mikoa hiyo kwa usimamizi mzuri wa maonesho hayo, na kuwatakiwa kila la kheri wananchi wote katika kushirki maonesho hayo. Maonesho ya 27 ya ya wakulima na wafugaji nanenane yatafikia kilele chake tarehe 8 agosti 2020.

Imeandaliwa na; Wilson Anatory

ETETA TV - MOROGORO  

Soma Zaidi

Habari na Matukio ya Nane Nane

Kuelekea Uzinduzi wa maonesho ya nanenane 2019 kanda ya mashariki - Morogoro.
Karibu kwenye Maonesho ya Wakulima Nanenane 2019 kanda ya mashariki Mkoani Morogoro
Maonesho ya nanenane 2019 KANDA YA MASHARIKI-MOROGORO

Wahisani

  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani