ETETA | Home juu

‘ZERO’ ZAPUNGUA MATOKEO KIDATO CHA NNE MKOANI MOROGORO

Jitihada mbalimbali za kitaaluma zinazoendelea kufanywa na wadau wa elimu ikiwemo viongozi, walimu, wazazi na wanafunzi zimeonesha kuzaa matunda bora mkoani Morogoro. Haya yamedhihirika katika matokeo ya kidato cha nne 2020 yaliyotangazwa hivi karibuni na Katibu Mkuu wa baraza la Mitihani la Taifa Dk. Charles Msonde.  

Katika kujali maendeleo ya watoto wetu, Idara ya Elimu Mkoa wa Morogoro imekuwa ikifanya tathmini ya ulinganifu wa ufaulu katika ngazi ya mkoa kwa kila mwaka matokeo yanapotangazwa.

Tathmini ya hivi karibuni ya matokeo ya kidato cha nne 2020 inaonesha kuongezeka kwa ufaulu katika daraja la kwanza hadi la nne huku idadi ya waliopata daraja sifuri ‘0’ ikipungua kwa kiasi kikubwa, ikilinganishwa na ufaulu wa mwaka 2019. Takwimu halisi kwa miaka hiyo miwili imeaninishwa katika jedwali hapo juu.

Tahimini ya jumla ni kuwa, ufaulu umeongezeka kutoka asilimia 78.82 kwa mwaka 2019 hadi kufikia asilimia 85.84 kwa mwaka 2020. Hii inamaanisha kuwa Mkoa wa Morogoro umefanikiwa kuongeza ufaulu kwa asilimia 7.02% ndani ya miezi 12 ya mwaka uliopita.

Katika upande mwingine, Idadi ya wanafunzi waliopata daraja sifuri ‘0’ imepungua kutoka 3,972 mwaka 2019 hadi kufikia 2,871 kwa mwaka 2020. Hii ni sawa na kusema kwamba, jumla ya wanafunzi 1,101 wameokolewa kutoka daraja sifuri kwenda katika daraja la kwanza hadi la nne ndani ya miezi 12 ya mwaka uliopita.

Pongezi nyingi zimwendee Mwalimu namba moja na Afisa Elimu Mkoa wa morogoro Eg. Joyce Baravuga kwa uongozi wake uliofanikisha yote haya katika mkoa wetu.  Pongezi zaidi ziwaendee viongozi wote wanaoshirikiana kwa pamoja katika kusimamia maendeleo ya elimu na watoto katika mkoa wetu akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Loata Ole Sanare, na Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Eng. Emmanuel Kalobelo.

Tunawapongeza Maafisa elimu Wilaya, Waratibu elimu na Wakuu wa shule kwa usimamizi wao mzuri wa shughuli za ufundishaji na ujifunzaji mashuleni.  Pongezi za pekee ziwaendee walimu wote mnaotumia muda wenu mwingi kuwaandaa watoto kwaajili ya mitihani ya taifa inayotupatia tathmimini za maendeleo kama hizi. 

Pamoja na ufaulu huo, changamoto kuu inabaki kuhakikisha tunaondoa daraja sifuri katika matokeo ya mkoa wetu wa Morogoro. Haipendezi na haifurahishi kuona mwanafunzi aliyeandaliwa kwa miaka minne shuleni kupata daraja sifuri ‘0’ ambalo ni fedheha kwa mwanafunzi husika, mwalimu hadi mzazi wake.

Katika suala la elimu, kila mmoja wetu anahusika. Kama wewe sio mwanafunzi, inawezekana unasomesha mtoto. Serikali kwa upande wake imeamua kutoa elimu bure. Nasi tuendelee kushirikiana pamoja ili kuunga mkono juhudi hizo za serikali katika kuhakikisha kuwa kila mtoto anayezaliwa ananufaika na elimu yetu  kwa kumwepusha kupata daraja sifuri maarufu kama ‘Division zero’.

Imeandaliwa na;

Mwl. Wilson Anatory

Kilakala Sekondari

Wahisani

  • Wahisani