ETETA | Home juu

Tafakari; SIKU YA WALIMU DUNIANI INANIKUMBUSHA WALIMU KAMA WAFUNGWA

(Pichani ni Mwl. Wilson Anatory akifundisha somo la Kompyuta kwa watoto wa darasa la tano katika moja ya shule za Msingi za Manispaa ya Morogoro)

Si vibaya kukumbuka mawazo ya kitoto niliyokuwa nayo. Nilipokuwa mdogo sikuwahi kufikiri kama ualimu ni ajira. Akili yangu ya kitoto ilinifanya niamini kuwa walimu ni watu waliofanya makosa ya jinai katika jamii, na hivyo kuhukumiwa adhabu ya kulea watoto wa wazazi wengine katika maisha yao yote. Yaaani mzazi akitaka kwenda kazini anawapeleka watoto wake wakashinde kwa mwalimu ili akawachukue jioni baada ya kazi.

Nilikuwa nikifanya ulinganifu kati ya maisha ya shule na yale ya nyumbani. Kwa kiasi kikubwa kulikuwa na uhusianao mkubwa wa malezi kati ya nyumbani na shuleni. Nikiwa shuleni au nyumbani niliweza kufundishwa mambo yaleyale kusoma, kuhesabu na kuandika. Kote huko nilihimizwa nidhamu, utii na bidii katika kazi.

Nikifanya kosa nyumbani, wazazi wangu walikuwa wanakasirika sana kiasi cha kuogopesha. Ilifikia hatua hadi nikawa naogopa kurudi nyumbani ninapogundua nimekosea. Hali ilikuwa hivyo hivyo hata kwa walimu wangu shuleni. Kuna wakati baadhi ya wanafunzi waliogopa kurudi shule kwasababu mwalimu fulani amekasirika na anawawinda kwa nguvu zote.

Kama haitoshi, walimu walionesha kukasirika zaidi kuliko hata wazazi wangu pale ninapoenda kinyume na utaratibu. Walikuwa tayari kusahau watoto wao ili kushughulika na watoto wa wazazi wengine.

Hilo lilitosha kuniaminisha kuwa walimu ni watu waliopewa adhabu ya kulea watoto kwa niaba ya wazazi wangu. Nisingeweza kudhani kwamba ualimu ni ajira waliyoomba wao wenyewe ili kulea watoto wa watu wengine.  Niliamini kuwa kile wanachokifanya ni kujihami ili adhabu waliyopewa isije ikaongezeka zaidi.  

Nikitazama hali za maisha yao ilikuwa ni uthibitisho wa mwisho kuwa ualimu ni adhabu iliyotolewa kwa wakosaji ili kulea watoto wa wazazi wengine wasio na makosa. Sikusita kuwafananisha na wafungwa walioko magerezani wanavyoamuka kwenda kusafisha mazingira na mitaro ya jiji wakati watu wengine wakienda kwenye biashara zao shughuli zingine za uzalishaji mali. Jioni wafungwa hurudi mikono mitupu wakati watu wengine wakirudi na mifuko iliyotuna.

Hadi namaliza kidato cha sita sikuwahi kuona kiyoyozi wala kiti cha kuzunguka shuleni. Walimu na wanafunzi walikuwa wanagombania viti na madawati yanayofanana. Walimu walikuwa wanatumia darasa mojawapo kama ofisi yao; nalo halikuwa na rangi wala hadhi ya kuitwa ofisi. Tumetoka mbali sana.

Katika baadhi ya shule, walimu walikuwa wanakosa hata maji ya kunawa mikono kuondoa vumbi la chaki baada ya kufundisha. Walilazimika kuja kunawa maji ya nyumbani yanayopatikana kwa shida. Achilia mbali umeme ambao wengi tulikuwa tunausoma tu vitabuni bila kujua ni kitu gani kinachozungumzwa. Hili si tatizo kwao kwakuwa walikuwa wanatekeleza kazi yao ya kulea watoto wa wazazi wengine walio ‘busy’ katika shughuli za uzalishaji mali.

Mwalimu akienda kazini, kulikuwa na uwezekano mkubwa wa pesa yake aliyoenda nayo mfukoni kurudi ikiwa imepungua au imeisha kabisa, tofauti na watumishi wengine ambao kuna uwezekano pesa aliyoenda nayo kazini kurudi ikiwa vile vile au imeongezeka zaidi. Ndiyo maana, mwalimu akistaafu kazi alikuwa kama mtu aliyemaliza kifungo chake jera. Alikuwa aidha hana nyumba kabisa au amejenga nyumba isiyo na hadhi kama watumishi wengine wafanyavyo. Elimu za watoto wake ilikuwa ni kama mchezo wa bahati nasibu.

Leo ninapokumbuka akili zangu za kitoto, Walimu wa zamani ninaomba sana mnisamehe kwa fikira hizo zilizoniplekea hadi kuwafananisha na wafungwa walioko gerezani.

Baada ya akili za utoto kunitoka, niligundua kuwa ualimu nao ni ajira rasmi tena yenye umuhimu mkubwa katika jamii. Ni kazi ambayo mtu husomea na kuomba kwa hiari yake mwenyewe. Infact, hata mimi nimeisomea pia. Kazi hii ni ya wito na ndiyo maana walimu wanaifanya kwa moyo sana bila kujali nini wanakipata kutokana na kazi hiyo. Wanaamini kuwa pale jicho la binadamu lisipofika, jicho la Mungu hufika.

Mwalimu ni kioo cha jamii. Kizazi cha kesho kinamtegemea mwalimu wa leo. Kama moja ya maadui wa nchi yetu ni ujinga, basi mwalimu ni silaha muhimu inayotegemewa kuangamiza ujinga katika Taifa. Kwa msingi huo, ipo sababu ya kuadhimisha siku ya Walimu duniani. Tuitumie kutafakari tulipotoka, tulipo na tuendako kama jamii inayomtegemea mwalimu.

Huwa ninaipenda sana kaulimbiu ya shule moja Mkoani Morogoro isemayo kuwa “The foundation of all Education is Love” ikimanisha kuwa “Msingi wa elimu zote ni upendo. Mtu anayekuelimisha anakupenda, vinginevyo angekuacha upotee. Bila upendo huwezi kuwa mwalimu. Utawafundishaje usiowapenda? Utakaaje na watoto wadogo wa watu wengine siku nzima na mwaka mzima kama huwapendi? Hongereni na poleni sana walimu wote mnaoendelea kupambana na ujinga katika nchi hii.  Leo ni siku yenu, muifurahie!

Mwalimu wa kwanza alikuwa ni Yesu Kristo. Mwaasisi wa taifa letu alikuwa ni Mwl. Nyerere. Hata kule Zimbabwe baba wa taifa lao alikuwa Mwl. Robert Mugabe ambaye pia alikuwa nguzo ya Afrika. Hii ni kazi takatifu na ya wito iliyotangulia kabla ya kazi zingine zote. Ni kazi inayozalisha fani zingine zote. Tuitende kwa moyo bila kujali changamoto zinazotukabili. Heshima kazi!

Ukikubali Wajibu, Timiza Wajibu!  

Imeandaliwa na;

Wilson Anatory

Kilakala Sekondari

Oktoba 05, 2020

Wahisani

  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani