ETETA | Home juu

SAUTI YA MWALIMU KWA MWANAFUNZI ANAYEJIANDAA KUFANYA MTIHANI WA TAIFA KIDATO CHA NNE 2020

Ni siku mbili tu zimesalia kabla ya mtihani wa Taifa kidato cha nne kuanza hapo jumatatu tarehe 23 Novemba 2020.

Kijana wangu ninaomba kusema nawe maneno machache kabla haujaingia kwenye chumba cha mtihani wako wa kuhitimu elimu ya sekondari. Kabla ya kuja kuongea na wewe, nilikuwa nawaza hali niliyokuwa nayo mimi zamani wakati nikijiandaa na mtihani kama huu ulio mbele yako. Katika kuwaza kwangu sikuishia hapo, pia nimeikumbuka ile taarifa ya habari ya TBC iliyoanza kwa mhitasari kuwa “Baraza la Mitihani la Taifa latangaza matokeo ya kidato cha nne kwa mwaka uliopita”. Hapo nimeshika kifua nikahamisika kusema na wewe haya machache;

1.      Mtihani ni utaratibu wa kawaida kabisa wa serikali zote katika kuchambua watu/wahitimu wake ili kujua nani mwenye sifa ya kuwa sehemu flani au kufanya kazi fulani. Tukiruhusu kila mtu ajichagulie kazi ya kufanya au sehemu ya kwenda baada ya kuhitimu masomo yake, baadhi ya kazi hazitapata watu; kazi moja itakimbiliwa na watu wengi kuliko inavyohitajika; baadhi ya kazi zitapata watu wasiostahili; na wengine watashindwa kabisa kuchagua kazi ya kufanya.   

 

Hoja yangu hapa ni kwamba, usiuogope mtihani ulio mbele yako. Wewe sio mkosaji na mtihani kama huo haujawahi kuwa miongoni mwa adhabu zitolewazo shuleni. Ni utaratibu wa kawaida kwa nchi zote. Ndiyo maana umeitwa mtihani wa taifa. Wanafunzi wenzako wote wa kidato cha nne Tanzania nzima watakuwa wanafanya mtihani huo huo unaoufanya wewe. Kama ulivyofaulu mtihani wa darasa la nne, la saba na kidato cha pili, amini kuwa utafaulu pia mtihani huu na kuendelea na hatua nyingine inayofuata.

 

2.      Nikikurejesha katika maisha ya Yesu kristo, wakati ule akiteua mitume wake 12 alikuwa anapita na kuchagua mtu kwa kumgusa tu na kumwambia nifuate bila kutoa mtihani. Huo ndio uliokuwa mtihani mgumu zaidi kwakuwa hapakuwa na nafasi ya kujitetea kwa wale ambao wangependa kuchaguliwa lakini hawakupata nafasi ya kuguswa.

 

Wewe una bahati kwakuwa utapewa kijitabu kizima (booklet) cha kujitetea ili uwe miongoni mwa watakaochaguliwa kuendelea mbele. Kama haitoshi, unaweza hata kuomba kijitabu cha ziada kadri ya uwezo wako ili tu kujitetea kiasi cha kutosha. Hakikisha unatulia na kujaza majibu sahihi na kutunza unadhifu wa kijitabu chako cha kujibia. Fuata sheria na maelekezo yote ya mtihani pamoja na wasimamizi wako. Fanya yako na Mungu atafanya yake kukusaidia.

 

3.      Mwisho, ukimaliza mtihani wako usiondoke nyumbani kabla hujaniona tena nikupe maelekezo kuhusu maisha yako baada ya kuhitimu shule. Una miezi mingi ya kukaa nyumbani kusubiri matokeo yako. Kwa yale ambayo mimi kama mwalimu sikuweza kukukufundisha kutokana na sababu mbalimbali, nitakushauri namna utakavyotumia muda wako kuendelea kujifunza ukiwa nyumbani.  

Wazazi wako wanakuombea mema na wanayo shauku kubwa ya kuona unafanikiwa vyema katika mitihani yako. Sote kwa pamoja tunakutakia kila la kheri ili uje kuwa miongoni mwa watakaochaguliwa kuendelea na ngazi zingine za elimu zinazofuata.

Ukikubali Wajibu, Timiza Wajibu!

 

Imeandaliwa na;

Mwl. Wilson Anatory

Kilakala Sekondari

Wahisani

  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani