ETETA | Home juu

Tafakari; MAISHA KATIKA DUNIA TATU

Jumatatu, tatu bora, tatu bomba, tatu mzuka, jiti tatu ni baadhi ya maeneo ambayo namba tatu imejizolea umaarufu. Kama haitoshi kuna watu wanaitwa Tatu. Ndio maana Dunia nazo ziko tatu ambazo usipozielewa vizuri utapata taabu sana kuziishi. Uzuri ni kwamba kila mmoja wetu ni lazima aziishi dunia hizo aidha kwa wakati mmoja au kwa nyakati tofauti tofauti. Wengi wetu huziishi kwa mtiririko kuanzia ya kwanza, pili na kumalizia na dunia ya tatu.

1.      Dunia inayotegemea nishati ya jua, nyota na mwezi

Dunia hii huwezi kuinunua wala kuimiliki lakini unaweza kuiona, kuigusa, kuionja au kuinusa. Angalau kila mtu kwa kiasi kikubwa anafahamu masharti ya kuishi dunia hii bila matatizo. Shule, katiba za nchi, NGO na taasisi mbalimbali zinafundisha masharti haya. Ikiwa hadi leo huna kesi ya jinai, na hauishi mafichoni, basi inawezekana umeshafuzu masharti ya kuishi dunia hii.

2.      Dunia inayotegemea nishati ya umeme tu

Dunia hii unaweza kuinunua na kuimiliki. Hii ni dunia inayokuwepo kwa msaada wa nishati ya umeme tu. Ukiondoa umeme dunia hii inatoweka kabisa. Hii ni dunia unayoweza kuiona kwa macho au kuisikia tu lakini huwezi kuigusa, kuinusa wala kuionja. Hii hupatikana kupitia simu zetu, Komputa na vifaa vingine vya teknolojia kwa msaada wa internet.

Maisha yaliyokamilika kabisa yanaendelea ndani ya dunia hii. Maisha haya yametokana na watu waliotoka dunia ya kwanza na kuamua kuhamia dunia ya pili. Dunia hii itakuwezesha kujua mwenzako anachowaza au anachofanya kwa wakati huo huo hata kama yuko nchi nyingine. Viongozi wanaitumia kuhutubia, wasanii kuburudisha, walimu kufundishia, wafanyabiashara kuuza, na wanafunzi kujifunza. Ni dunia unayoweza kutembea nayo mfukoni au kiganjani.

Changamoto kubwa ya dunia hii, inakuwa na taarifa nyingi sana ambazo zinabaki kuwachanganya au kuwapoteza watu badala ya kuwasaidia. Pili, dunia hii inaathiri sana maisha katika dunia ya kwanza. Kuna wengi wameharibikiwa, wamerubuniwa, wamedanganyika, wametapeliwa, wameibiwa, wametekwa na kupotezwa kutokana na kutojua masharti ya kuenenda katika dunia ya pili.

Muhimu zaidi  ni kwamba, nenda dunia ya pili ukiwa tayari umeshaamua nini unachokitafuta pale. Bila hivyo, utapoteza muda na nguvu yako ya kutosha huku ukiambulia patupu. Tumia maisha unayoyaona pale kama hamasa kwako lakini yasikuumize na usiyaamini sana kwakuwa si wakati wote yatakuwa maisha halisi.

 

3.      Dunia isiyotumia nishati ya jua, nyota, mwezi wala umeme

Dunia hii huwezi kuinunua wala kuimiliki. Hii ni dunia ya kufikirika. Ni ulimwengu wa kiroho. Ili ufike huko, ni lazima uachane na dunia zote mbili zilizotangulia. Masharti ya dunia hii hufundishwa katika nyumba za ibada na kwa watumishi wote walioandaliwa kutoa huduma za kiroho. Tarifa nzuri ni kwamba unaweza kutumia dunia ya kwanza na ya pili kujifunza mambo yatakayokuongoza katika njia sahihi kuelekea dunia ya tatu. Dunia hizo hizo mbili usipozitumia kwa makini, ni sababu tosha ya kupotea njia sahihi kuelekea dunia ya tatu.

Ukizielewa dunia zote tatu haikupi tabu; Jitahidi kuzifahamui aina za binadamu katika kila dunia ili ujue namna ya kuishi. Si unajua bora wali-maharage kuliko wali-mwengu?!!

Ukikubali Wajibu, Timiza Wajibu!

Imeandaliwa na;

Wilson Anatory

Kilakala Sekondari

Wahisani

  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani