ETETA | Home juu

AFISA ELIMU MKOA WA MOROGORO ATEMBELEA MAONESHO YA NANENANE, ATOA ZAWADI KWA WATUMISHI WA IDARA YA ELIMU MANISPAA YA MOROGORO

(Pichani ni Afisa Elimu Mkoa wa Morogoro Eng. Joyce Baravuga (wa pili kutoka kulia) akiwa na watumishi wa Idara ya Elimu Msingi na Sekondari Manispaa ya Morogoro katika maonesho ya nanenane yanayoendelea mkoani Morogoro)

Inawezekana wewe si mwanafunzi lakini unasomesha watoto. Hii ina maana kwamba  kila mtu anahusika na suala la elimu kwa namna moja au nyingine. Mwalimu makini hupenda kukagua kazi na maendeleo ya wanafunzi wake kila mara ili kuboresha mbinu za ufundishaji wake. Hiki ndicho alichokifanya Afisa Elimu Mkoa wa Morogoro Eg. Joyce Baravuga kiongozi na mwalimu namba moja mkoani Morogoro.

Mapema leo tarehe 7 agosti 2020, kiongozi huyo alitembelea maonesho ya wakulima na wafugaji maarufu kama nanenane.  Kwa kuzingatia kuwa kila mkulima na mfugaji alipita kwenye mikono ya mwalimu kabla ya kujiingiza kwenye ajira hiyo, Eng. Baravuga ametembelea maonesho kama mwalimu anayekagua matunda ya kazi yake. Ilikuwa ni ya muhimu sana kwake kufanya hivyo kwakuwa ndiye mwenye sauti ya kushauri maboresho yanayohitajika katika kuandaa wahitimu walio bora kulingana na mahitaji ya nchi. Katika hili, anastahili pongezi kwa kutimiza wajibu wake.

Baada ya kutembelea na kujifunza katika vipando na mabanda mbalimbali ya maonesho, aliwasili katika banda la Idara ya Elimu Manispaa ya Morogoro ambapo alifanya kitu kitakachobaki kwenye kumbukumbu za watumishi wa idara hiyo waliokuwa wakihudumu hapo.  

Mara baada ya kuwasili aliomba kupewa maelezo kama mteja mwingine wa kawaida. Wahudumu waliokuwa wakionesha kujiamini, walieleza kwa umahili mkubwa na kujibu maswali yote yaliyoulizwa na kiongozi huyo. Walimshirikisha kucheza michezo mbalimbali ya chemsha bongo inayotumika kufundishia watoto shuleni na kila mmoja alifurahi sana.  

Eng. Baravuga alionesha kuridhika na maonesho hayo, akaamua kuwapongeza na kutoa zawadi kwa wahudumu wote 15 waliokuwepo hapo kutokana na kuiwakilisha vyema idara ya Elimu Msingi na Sekondari  katika maonesho hayo.  

Nao wahudumu walifurahi sana kwa namna kiongozi wao alivyoridhika na kazi yao hadi kuwazawadia. Waliamua kupiga naye picha ya pamoja kwaajili ya kumbukumbu, huku kila mmoja akipambana kupata picha binafsi ya kumbukumbu akiwa na kiongozi huyo.

Ikumbukwe kuwa, moja ya vitu vilivyokuwa vikioneshwa hapo ni video zilizorekodiwa za masomo ya shule za msingi na sekondari kwa usimamizi wa Idara hiyo. Video hizo ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya ‘Elimu kwa Tehama Tanzania (ETETA) iliyoasisiwa na Eng. Baravuga kama Afisa Elimu Mkoa wa Morogoro tangu mwaka 2018.

Hii ni sera inayolenga kuufanya mkoa wa Morogoro kuwa wa kidijitali ifikapo mwaka 2022 kwa kuongeza matumizi ya Tehama katika taasisi za elimu na nyinginezo.  Video hizo za masomo zinaweza kupatikana katika mtandao wa youtube channel ya ETETA TV inayopatikana ukiwa mahali popote pale ndani au nje ya nchi. Katika maonesho hayo, video hizo zinatolewa bure kwa wananchi wanaofika hapo wakiwa na ‘flash disk’ za kuhifadhia.

Maonesho hayo ya kanda ya mashariki yanahusisha mikoa ya Morogoro, Pwani, Dar es Salaam na Tanga yakiwa na kaulimbiu isemayo kuwa; “Kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi chagua Viongozi bora 2020.

Imeandaliwa na; Wilson Anatory

ETETA TV - MOROGORO

Wahisani

  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani