ETETA | Home juu

‘ETETA TV’ TUACHE KUFUNDISHA KIDIGITALI KWASABABU BAADHI YA WANAFUNZI/WAZAZI HAWANA AU HAWAJUI KUTUMIA SIMU JANJA?

(Pichani ni walimu wa shule za msingi na sekondari manispaa ya Morogoro wakipatiwa mafunzo juu ya Elimu mtandao yaliyofanyika mwezi june katika shule ya sekondari Morogoro)

Mdau anasema “Mimi nina mashaka na mnachotaka kukifanya kama kitafanikiwa na kuwafikia walengwa au mnataka kufanya kujifurahisha tu?” Ameongeza kuwa wanafunzi waliwahi kuwekewa utaratibu wa kuwawezesha kubadilisha tahasusi zao mtandaoni. Pamoja na kuwa iliwahusu wale waliokwishahitimu kidato cha nne lakini walionekana kushindwa kutumia mtandao na hivyo kufanyiwa kazi hiyo na walimu au watu wanaotoa huduma za mtandao ‘internet café.’.

Anaendelea kuhoji kuwa, wazazi wote wana simu janja? Walionazo watawaachia watoto wazitumie kusoma? Wana bando za kupata mtandao? Kwa utafiti gani kupitia ‘whatsap’ masomo yatawafikia wanafunzi?

--------Upi ni mtazamo wa Mwalimu Wilson Anatory katika hilo? Endelea!

Kila kitu lazima kiwe na mwanzo wake, ETETA TV tumeanza!

Zamani niliamini kuwa waafrika tunapendana sana kwasababu tunasalimiana kwa kushikana mikono, lakini Corona ilipofika kwetu, tuliambiwa tusishikane mikono wala kusogeleana na maisha yaliendelea kama kawaida. Swali ni je, tukiacha kushikana mikono tutakuwa hatupendani tena?

Kwa nchi za wenzetu zenye baridi na uchafuzi mkubwa wa hali ya hewa, Barakoa kwao zilijulikana na kutumika hata kabla ya korona. Walianza kuzitumia zamani kwasabu wana tabia ya kujali afya zao tofauti na kwetu unapoweza kukuta vijana wakipakua mifuko ya Cement kwenye Lori bila hata ya barakoa.  Huku kwetu, neno barakoa halikufahamika kabla ya mwaka 2020. Lakini leo kila duka linauza barakoa na tunazitumia.

Pamoja na ubaya wa Corona yapo mazuri ambayo yameibuka na yataendelea kuibuka  wakati huu. Haya hatutayaacha kamwe kwasabbu tumeshaonja ladha yake nzuri tuliyokuwa tumechelewa kuifahamu.  

Ni ukweli usiopingika kuwa wapo baadhi ya wazazi/wanafunzi wasiomiliki simu janja. Wapo wanaozimiliki lakini kipato ni kidogo kununua bando kila siku. Wapo pia ambao hawajui kabisa kutumia mtandao. Lakini pia tukubaliane kuwa wapo wazazi na hata wanafunzi wengi wanaomiliki simu janja hapa hapa Tanzania. Je, kwasabu wachache hawana hizo simu janja tuache kufundisha kidigitali ili wakose wote?  

Naomba ifahamike kuwa, katika muda mfupi ujao, teknolojia itakuwa kitu cha lazima na sio ombi au anasa. Kwenye somo la baiolojia tunasema “Survival for the fitest”. Utaamua kutumia teknolojia uishi au usitumie ili utoweke duniani mapema.

Duniani kote, Corona imechochea matumizi ya Tehama katika kila nyanja ya maisha ikiwemo elimu. Haijalishi kuwa ni wangapi watafikiwa kwa hapa mwanzo. Kinachotakiwa ni kuianza safari na wengine wataendelea kujiunga na safari hiyo njiani. Safari hii ni ndefu.

Tambua kuwa, wapo ambao hawakuwahi kumiliki simu janja kwasababu hawajaona ulazima huo; ni wakati wao kununua. Yupoo mzazi aliyekuwa hana sababu za kumpa simu mtoto wake kwasababu hakuamini kama simu inaweza kutumika kujifunzia masomo, sasa imani italazimika kuja. Yale makatazo ya mwanao usimzoweshe kushika simu yanaenda kuwa zilipendwa. Ulikuwa unamnyima simu isiyo hata na salio la maongezi, sasa utalazimika mwenyewe kumwekea salio la maongezi pamoja na bando la kuingia mtandaoni, kisha kumpunguzia sauti ya redio yako ili ajisomee.

Tutakuwa watu wa ajabu sana kama tutaacha kufundisha wale wanaofikia mtandao hata kama ni wachache eti kwa sababu wengi hawana simu. Hakuna siku ambayo mazingira yote yatakuwa sawa kwa asilimia 100 ili tuanze. Ina maana yule asiye na simu leo aliumbwa kutomiliki simu milele? Yule asiye na bando leo aliumbwa kutomiliki bando milele? Yule asiyejua kutumia mtandao aliumbwa kutojua milele?

Kwa bahati nzuri mwanafunzi halazimiki kusoma wakati fulani pekee. Wakati wowote atakapokuwa tayari atayakuta masomo yakimsubiri mtandaoni. ETETA TV kupitia Idara ya Elimu Mkoa wa Morogoro kitengo cha TEHAMA imedhamiria kuufanya mkoa wa Morogoro kuwa wa kidijitali ifikapo mwaka 2022.

Masomo yote ya shule za msingi na sekondari  kuanzia mada ya kwanza hadi ya mwisho yatarekodiwa na kuhifadhiwa kwenye mtandao wa ETETA TV pamoja na mifumo mingine kama CD.  Malengo yetu sio kusaidia wanafunzi kipindi hiki cha Corona pekee bali kufanya TEHAMA kuwa sehemu ya maisha yetu ya kila siku shuleni na nyumbani. Ukishindwa kuungana nasi leo, kesho utatukuta. Kawia lakini ufike.

Tunawaomba walimu, wazazi na walezi kuunga mkono jitihada hizi ili kusaidia watoto wetu wazoee na wasome bila shida kidijitali kupitia ETETA TV. Saidia kutatua changamoto yoyote iliyo ndani ya uwezo wako. Siku kila mtu akifagia uwanja wake, dunia nzima itakuwa imefagiliwa.

Imeandaliwa na; Wilson Anatory

ETETA TV - MOROGORO

Wahisani

  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani