ETETA | Home juu

MANISPAA YA MOROGORO YAZIPIGA 3 BILA HALMASHAURI ZA MIKOA MINNE YA KANDA YA MASHARIKI MAONESHO YA NANENANE 2020

Inawezekana wenzetu wanatamani tushangilie kimyakimya ili isijulikane kama tumewashinda, lakini watusamehe kwakuwa tunashindwa kuficha hisia zetu. Ungekuwa ushindi wa kawaida tungepunguza sauti, lakini kwa ushindi huu wa tatu bila; Morogoro piga Keleleeeeee!!!  

Siku ya jana tarehe 8 Agosti 2020 maarufu kama siku ya nanenane ilikuwa njema kwetu wana Morogoro baada ya halmashauri yetu ya manispaa ya Morogoro kuibuka mshindi wa kwanza katika vipengele vyote vitatu wakati wa kilele cha maonesho ya nanenane yaliyokuwa yakifanyika mkoani Morogoro.  Halimashauri ya Manispaa ya Morogoro imejitwalia jumla ya tuzo tatu baada ya kuzishinda halmashauri, manispaa na majiji yaliyopo katika  mikoa minne ya kanda ya mashariki ikiwemo Morogoro, Pwani, Dar es Salaam na Tanga.

Manispaa ya Morogoro ambayo ndiyo mwenyeji wa maonesho hayo, imekuwa mshindi wa kwanza katika vipengele vifuatavyo; (1) Kundi la Manispaa na Majiji yote ya mikoa minne, (2) Mshindi katika Halmashauri za mkoa wa Morogoro na (3) Mshindi katika maonesho ya kikanda (Kanda ya mashariki).  

Tuzo hizo zilitolewa na Waziri wa Afya maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto Mhe. Ummy Mwalimu ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi katika kilele cha maonesho ya nanenane kanda ya mashariki.

Dalili za ushindi huo zilionekana tangu mwanzo wa maonesho hayo ambapo Manispaa ya Morogoro ilikuwa imejipanga kikamilifu kuhakikisha inakuwa mshindi. Wakati maonesho yalipoanza, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Bakari Msulwa alitembelea mabanda ya halimashauri ya Manispaa Morogoro ambapo alisistiza mambo makuu mawili. “Kazi zetu kuu ni mbili katika maonesho haya; kwanza ni kuhakikisha ushindi unabaki nyumbani kwetu, pili ni kuhakikisha haya mambo mazuri tunayoyaonesha yanafanyika kivitendo huko kwa wakulima na siyo kuishia hapa kwenye viwanja vya maonesho tu”. Alisema Mhe. Msulwa.   

Bila shaka, ushindi huu mkubwa umekata kiu hiyo aliyokuwa nayo Mkuu wa wilaya ya Morogoro pamoja na viongozi wote waliohusika kuratibu na kusimamia maonesho hayo. Ushindi huo unaongeza chachu kwa wakulima wa halmashauri ya Manispaa ya Morogoro na hata wale wa wilaya zingine za Mkoa wa Morogoro ikizingatiwa kuwa mkoa huo ni ghala la taifa la chakula.  

Maonesho ya nanenane ya mwaka huu yaliongozwa na kaulimbiu isemayo; “Kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Chagua Viongozi bora 2020”. Kumalizika kwa maonesho hayo ni mwanzo wa kujiandaa na maonesho mengine ya nanenane kwa mwaka ujao 2021. Manispaa ya Morogoro ndiyo sisi, tatu bila zingine zinakuja!

Imeandaliwa na; Wilson Anatory

ETETA TV - MOROGORO   

Wahisani

  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani