ETETA | Home juu

UKIJA NA UBUNIFU TUTAUPOKEA, TUTAKUTANGAZA NA TUTAKUENDELEZA - REO MOROGORO

(Pichani ni washiriki wa mafunzo na uzinduzi wa programu ya Elimu mtandao (Teschool) iliyobuniwa na taasisi ya APPS AND GIRLS na kuzinduliwa Mkoani Morogoro)

Mapema wiki hii ilikuwa siku ya uziduzi wa programu ya kufundishia elimu mtandao (Teschool) iliyobuniwa wa taasisi binafsi ya APPS AND GIRLS ya Dar es Salaam.

Uzinduzi huu uliofanyika tarehe 28/8/2020 katika shule ya sekondari Morogoro iliyopo katika halimashauri ya Manispaa ya Morogoro, ulihudhuriwa na Afisa Elimu Mkoa wa Morogoro Eng. Joyce Baravuga kama mgeni rasmi akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Loata Erasto Ole Sanare. Viongozi wengine walioshiriki Afisa Elimu Manispaa ya Morogoro Dkt. Janeth Balongo, ndugu Mussa Mnyeti – Afisa Elimu Taaluma mkoa wa Morogoro, ndugu Enock Juliely – Afisa Elimu Taaluma Tehama na maafisa wengine wa Idara za elimu.

Kabla ya uzinduzi huo, yalitangulia mafunzo ya namna ya kutumia programu hiyo (Teschool) kwa waratibu elimu, wakuu wa shule, walimu wa TEHAMA na wanafunzi.

Akitoa hotuba ya uzinduzi, Eng. Baravuga aliwashukuru watendaji mbalimbali katika Idara ya elimu Mkoa kwa kuikubali na kuisimama vyema sera ya Elimu kwa TEHAMA iliyoasisiwa na kiongozi huyo tangu mwaka 2018.

Alitaja na kuwapongeza watendaji kadhaa wa Idara ya Elimu Mkoa wa Morogoro walioonesha ubunifu na uwezo mkubwa katika kutekeleza sera na mipango ya Idara.

'Kwa mfano, huyu Enock Juliely alikuwa ni mwalimu wa kawaida tu huko Morogoro vijijini, lakini aliposikia tumeanzisha mpango huu wa Elimu kwa Tehama Tanzania (ETETA alisafiri toka huko hadi ofisini kwangu akaniletea mapendekezo mazuri sana ya namna ya kuutekeleza.  Kwakweli niliyapenda sana na leo hii ameendelea kuwa msaada sana katika Idara ya Elimu Mkoa akiwa Afisa Elimu Taaluma Tehama'. Alisema Eng. Baravuga.

Pia, aliwasihi watendaji wa ngazi zote kuanzia shule, kata, halmashauri hadi mkoa kujiwekea utaratibu wa kupeana taarifa ya maendeleo ya Elimu kwa Tehama kila mwezi ili kila mtu ajue kinachoendelea katika shule za mkoa wa Morogoro.

'Taarifa ianzie kwa Mwalimu wa Tehama shuleni ipitie kwa Mkuu wa Shule kwenda kwa Mratibu Elimu kata, Afisa Elimu Manispaa hadi kwa Afisa Elimu Mkoa. Na kila ngazi ibaki na nakala yake' Alisema Eng. Baravuga.

Aidha aliwataka walimu na viongozi wote katika sekta ya elimu kuwa wabunifu ili kuchangia mafanikio ya ETETA na kuongeza ufaulu wa wanafunzi. 'Yeyote atakayetuletea ubunifu wowote mzuri tutaupokea, tutamtangaza na tutamwendeleza' Alieleza Eng. Baravuga.

Katika hatua nyingine alimpongeza Mkurugenzi wa APPS AND GIRLS ndugu Carolyne Ekyarisiima kwa ubunifu wa masuala ya TEHAMA uliopelekea kuanzisha taasisi hiyo akiwa kama mwanamke. Pia, alimpongeza kwa ubunifu wa programu hiyo ya kufundishia (Teschool) na hata kuamua kuizindulia mkoani Morogoro. Ninafahamu ugumu wa kazi hii nikiwa kama Injinia wa TEHAMA. Hongereni sana kwa kazi nzuri mnayofanya. Alisema Eng. Baravuga.

Ilielezwa kuwa baada ya uzinduzi huo vilabu vya  TEHAMA (ICT Clubs) zitaanzishwa mashuleni chini ya usimamizi wa APPS AND GIRLS kwa kushirikiana na Idara za elimu mkoani Morogoro. “Kutoka katika idara yangu Mkoani, tayari nimeshapanga walezi kwenye kila wilaya ya Morogoro ili kuhakikisha Elimu kwa TEHAMA inafanikiwa”. Alieleza Eng Baravuga.

Hii imekuwa hatua nyingine ya kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya APPS AND GIRLS na Idara za Elimu Mkoani Morogoro.

Zaidi ni kuwa mpango wa Elimu kwa Tahama Tanzania (ETETA) Ulioasisiwa na Afisa Elimu mkoa wa Morogoro Eng. Baravuga imezidi kupata msukumo mkubwa kutokana na washirika mbalimbali wanaojitokeza kushiriki katika juhudi hizo. Tulipanga kuufanya mkoa wa kidijitali ifikapo mwaka 2022, naona sasa kama tumeanza kufika kabla hata ya wakati. Alisema Eng. Baravuga

Kama kawaida yake ya ucheshi Eng Baravuga alihitimisha hotuba yake kwa kuwatania washiriki kwamba, waende wakadumishe upendo katika nyumba zao ili ETETA izidi kufanikiwa. “Kila mweye ujuzi kidogo wa TEHAMA amfundishe mtu wake wa karibu ndani kwake. Mke mfundishe mme na Mme mfundishe mke au hata rafiki. Mimi nilimfundisha TEHAMA Mme wangu akafanya vizuri hadi wakaanza kumuita Mr. IT (Information Technology). Si mnajua ukitoka nyumba yenye upendo hata kazini unafanya vizuri?

Imeandaliwa na; Wilson Anatory

ETETA TV -MOROGORO

Wahisani

  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani