ETETA | Home juu

RAS, REO - MOROGORO WAMTABIRIA MTOTO CHARLES MATHIAS KUWA MHANDISI MWENYE UMRI MDOGO ZAIDI TANZANIA

Katika siku za hivi karibuni, video inayoendelea kusambaa kwa kasi katika mitandao ya kijamii ni ile ya mtoto mdogo Charles Mathias Mbena (6) aliyegundulika kuwa na kipaji kisicho cha kawaida cha kukokotoa hesabu zisizoendana na umri wake kwa kutumia kichwa chake. Hahitaji kikokotoo wala Kompyuta.

Mtoto Charles ambaye ana miezi miwili pekee shuleni akiwa amesajiliwa kama mwanafunzi wa darasa la awali/chekechea mwaka huu 2021, amekuwa gumzo mitandaoni hali iliyowavutia viongozi wakubwa na wadau mbalimbali wa malezi na elimu kufika shuleni kwake kumtia moyo na kumsaidia kuendeleza kipaji chake.

Katika video iliyoambatanishwa na makala hii, ni Katibu tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo pamoja na Afisa Elimu Mkoa wa Morogoro Mhadisi Joyce Baravuga walioambatana na viongozi na wadau wengine katika ziara ya kwenda katika shule ya Msingi Nyingwa iliyopo katika Wilaya ya Morogoro Vijijini anakosoma mtoto Charles Mathias.

Jambo linalotia moyo zaidi ni namna viongozi hao wakubwa walivyoamua kuacha shughuli zao kwaajili ya kumfikia mtoto Charles Mathias katika kijiji ambacho hata magari yao yalishindwa kupita katika baadhi ya maeneo na hivyo kulazimika kutembea kwa miguu.

Mhandisi Kalobelo aliagiza mtoto Charles kuvushwa darasa kutoka chekechea hadi darasa la kwanza wakati taratibu zaidi zikiendelea kufanyika za kumwendeleza mtoto huyo. Alisisitiza kuwa ni lazima mtoto Charles atafutiwe makao mengine yatakayokuza kipaji chake. 'Rais wetu John Pombe Magufuli kila siku anasisitiza Tanzania kuwa nchi ya viwanda, ni lazima tutambue na kuendeleza vipaji hivi ili baadaye tuwe na wanasayansi wakubwa wazawa. Si lazima wagunduzi wote watoke nje ya nchi'. Alisema Mhandisi Emmanuel Kalobelo.

Mtoto Charles alizawadiwa zawadi za kitaaluma zinazoweza kusaidia kumchangamsha zaidi akili ikiwemo mpira wa miguu, daftari na vifaa vya kuchorea.

Katibu tawala alieleza kuwa, wafadhiri wengi wamejitokeza kumsaidia mtoto Charles na hivyo kuwaomba wazazi wa mtoto huyo kutoa ushirikiano kwakuwa ni kwa nia nzuri ya kumwendeleza Charles.

Baadhi ya wafadhiri hao ni pamoja na Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro (Mjini) aliyetoa nafasi katika shule maalumu ya Manispaa inayofundisha kwa lugha ya kiingereza (English medium school). Pia, Mhandisi Kalobelo alimtambulisha mwakilishi wa kanisa la Full Gospal la Dar es Salaam waliojitolea kumsomesha mtoto Charles hadi atakapomaliza elimu ya shule ya msingi.

 

Katibu tawala alimwagiza Afisa Elimu kuratibu mambo yote hayo kwa haraka inavyowezekana ili mtoto Charles asikwame.

Pia aliagiza majengo yanayoendelea kujengwa katika shule hiyo yakamilike haraka iwezekanavyo na mengine mapya yaanze kujengwa ili kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa watoto wote wanaobaki shule hapo. 'Wanafunzi nawaomba msijikatie tamaa, ni mazingira kama haya haya na sisi tumetoka hadi tumekuwa wahandisi na viongozi katika serikali'. Alisema Mhandisi Kalobelo.

Naye Afisa Elimu Mkoa wa Morogoro Mhandisi Joyce Baravuga alimpongeza Katibu tawala kama Kiongozi wa kwanza Mkubwa kufika shuleni hapo na kuahidi kumsimamia vyema mtoto Charles. 'Mimi ni Mhandisi, Katibu tawala naye ni Mhandisi; tumekuja kumtembelea mhandisi mdogo mpenda mahesabu. Ninamwombea aje kuwa mwanasayansi Mhandisi mdogo zaidi Tanzania'. Alisema Mhandisi Baravuga.

Pia waliwapongeza walimu na wathibiti ubora wa shule ambao ndio walioibua kipaji cha mtoto Charles. Zaidi aliwapongeza wazazi wa mtoto Charles kwa malezi mazuri akiahidi kuwasaidia katika kufanikisha ndoto za mtoto Charles.

Kwa pamoja, viongozi hao waliwataka walimu na wazazi kuendelea kutambua na kuibua vipaji wa watoto ili kuvilea kwa manufaa ya taifa letu la Tanzania.

Baba yake mtoto Charles Bw. Mathias Mbena aliwashukuru viongozi hao kwa kufika kijijini kwao kwaajili ya mtoto wake Charles kitendo ambacho yeye hakukitegemea kutokea. 'Nilikuwa ninaambiwa na watu wenye simu kwamba wamemwona mwanangu kwenye mitandao ya whatsap na runinga. Ninafurahi sana kuona mkifika hapa kutokana na kipaji cha mwanangu. Ninaamini kwamba akiendelezwa ataweza kuja kuwasaidia na watu wengine'. Alisema Bw. Mbena.

Kujionea tukio zima, fungua link hii https://youtu.be/aVLhSX5MHEI  

Imeandaliwa na;

Mwl. Wilson Anatory

Kilakala Sekondari

Wahisani

  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani