PROGRAMU YA ‘WATOTO WETU TUNU YETU’ KUWANUFAISHA WATOTO WENGI ZAIDI MKOANI MOROGORO
(Pichani ni viongozi kutoka mashirika yanayojihusisha na watoto ya CIC na CDO pamoja na viongozi mbalimbali wa Elimu Mkoani Morogoro walipotembelea wanafunzi wa darasa la awali katika shule ya Msingi Ngai iliyoko katika kata ya Mchombe Wilayani Mlimba Mkoani Morogoro tarehe 24/5/2021)
Moja ya kitu tunachojivunia hapa kwetu Morogoro ni uwepo wa taasisi (NGOs), Mashirika na watu binafsi wanaofanya kazi kwa kushirikiana na serikali katika kuwahudumia watanzania. Unakumbuka jinsi taasisi na wadau wa elimu walivyogombania fursa ya kumwendeleza mtoto Charles Mathias aliyegundulika kuwa na kipaji katika hisabati akiwa darasa la awali huko halmashauri ya Morogoro vijijini?
Leo tutawazungumzia wadau wetu wengine wa elimu ambao kwa nafasi yao wameweza kufanya makubwa sana katika kuunga juhudi za serikali za kuwahudumia wananchi hasa katika utoaji wa elimu ya awali. Ni nani hao na wamefanya nini kuwanufaisha watoto wetu? Majibu yote ni katika aya zifuatazo.
Mwaka 2018, Shirika la kimataifa la ‘Children in Crossfire (CIC)’ lenye ofisi zake jijini Dar es Salaam kwa kushirikiana na taasisi nyingine ya wazawa ya ‘Children Development Organization, (CDO)’ ya Morogoro waliomba kushirikiana na serikali katika kutoa maandalizi mazuri ya watoto wadogo kwaajili ya kujiunga na darasa la kwanza. Mashirika yote hayo mawili yana malengo yanayofanana ya kusimamia malezi na maendeleo mazuri ya watoto wadogo kati ya miaka 3 hadi 6. CIC na CDO wanaamini kwamba ili mtoto afanikiwe katika taaluma za madarasa ya juu ni lazima ajengewe msingi bora wa malezi kupitia elimu ya awali.
Mashirika hayo hulenga zaidi maeneo ya vijijini ambako watoto wengi hukosa fursa ya elimu ya awali na kupitia changamoto nyingi zinazoathiri makuzi na maendeleo yao. Katika kutimiza wajibu wao, CIC na CDO hufanya mambo yafuatayo;
i) Kuhamasisha uanzishaji wa vituo vya watoto (day care centers) vya kijamii vyenye gharama nafuu kwa mzazi kulipia.
ii) Kutoa mafunzo ya utoaji wa elimu ya awali kwa walimu, wakuu wa shule, maafisa elimu wilaya na kata, viongozi wa kijiji, wazazi nk.
iii) Kufadhiri vifaa vya kufundishia na kujifunzia kwa watoto wadogo kama vile makabati ya kutunzia vifaa, penseli, vitabu, michoro nk.
iv) Kusimamia masuala ya lishe na usalama wa mtoto.
v) Kuboresha miundombinu ya darasa la awali.
vi) Kulea vituo vilivyoanzishwa na kutengeneza mifumo ya kuweza kujiendesha hata baada ya wao kuondoka.
vii) Kufanya tathmini na kushauri serikali juu ya mabadiliko au maboresho ya sera zinazosimamia watoto yanayohitajika kutegemeana na mahitaji ya wakati uliopo.
Kwa sasa CIC na CDO wanafanya kazi katika mikoa miwili pekee ambayo ni Dodoma na Morogoro. Kwa hapa kwetu Morogoro wamekuwa wakifanya kazi katika wilaya za Mvomero, Ifakara na Mlimba tangu mwaka 2018 ambapo mradi huo unatarajiwa kukamilika mwaka 2022.
Kuanzia tarehe 24 hadi 27/5/ 2021, viongozi wa CIC na CDO walikuwa wakifanya tathmini ya mafanikio yaliyopatikana katika programu yao kwa muda wote tangu walipoanza. Miongoni mwa viongozi hao alikuwa ndugu Heri Ayubu ambaye ni Msimamizi Mkuu wa Mipango na uendeshaji pamoja na Frank Samson kutoka shirika la CIC. Wengine ni ndugu Marsel Salema na Joseph Machira ambao ni viongozi kutoka CDO. Viongozi hao waliambatana na Mwl. Wilson Anatory ambaye ni Afisa kutoka Idara ya Elimu Mkoa aliyemuwakilisa Afisa Elimu Mkoa wa Morogoro Eng. Joyce M. Baravuga.
Zoezi hili lilifanyika kwa kutembelea Wilaya za Mlimba na Ifakara na kukagua vituo vilivyokuwa vikinufaika na programu hiyo pamoja na vile visivyonufaika ili kupata ulinganifu. Pia, walizungumza na Maafisa elimu Wilaya na Kata, Maafisa wa ustawi wa jamii, kamati za shule, wazazi, walimu wakuu wa shule na walimu wa darasa la awali katika shule husika.
Shule zilizotembelewa ni pamoja na Shule ya Msingi Ngai iliyopo katika kata ya Mchombe na shule ya msingi Ngajengwa iliyopo katika kata ya Igima zote Wilayani Mlimba. Pia walitembelea kituo cha watoto wadogo (day care school) cha Mt. Yohana kilicho chini ya kanisa katoliki Mlimba. Shule nyingine ni Shule ya msingi Darajani iliyopo katika kata ya Mwaya Wilayani Ifakara pamoja na kituo cha watoto cha Upendo kilichopo katika wilaya hiyo.
Kwa ujumla wadau wote hapo juu walionesha kufurahia programu hiyo kwakuwa imesaidia watoto wengi kuwa katika mikono salama ya walimu badala ya kuachwa mitaani ambako hakuna uhakika wa kesho yao.
Wazazi wengi wamehamasika kuchangia maendeleo ya watoto wao na hata kushiriki shughuli ndogondogo za kuandaa zana za kufundishia watoto kwa kushirikiana na mwalimu wa darasa la awali. Kamati za shule zimeweza kujitengenezea mpango kazi unaowaongoza katika mipango yao ya mwaka ya uendelezaji wa shule na watoto.
Walimu wa madarasa ya awali kwa kushirikiana na walimu wakuu wa shule wameweza kuboresha mandhari ya madarasa ya awali kuwa na muonekano unaoshauriwa kitaalamu kwa kupanga sehemu kuu za darasa kama vile sehemu ya kusomea vitabu, sehemu ya kuandikia, sehemu ya kucheza, sehemu ya kufanyia sanaa nk. Pia, madarasa yamepambwa vizuri kwa picha na maandishi ya kujifunzia watoto kama inavyoshauriwa kitaalamu.
Katika majumuisho ya ziara hiyo yaliyomshirikisha Afisa Elimu Msingi halmashauri ya Mji Ifakara ndugu Sylvester Kalagile pamoja na Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Darajani, viongozi wa CIC na CDO walishukuru sana kwa ushirikiano walioupata tangu siku ya kwanza hadi ya mwisho katika ziara yao ya kufanya tathmini. Walionesha kufurahishwa na jinsi wazazi walivyoitikia uhamasishaji wao na kuwezesha shule kujisimamia zenyewe.
Sambamba na hilo, walitoa wito kwa viongozi wa elimu wakiwemo Maafisa elimu Wilaya na kata, walimu wakuu wa shule na wadau wengine kujifunza na kuhamisha mambo mazuri yaliyo katika shule zilizonufaika na programu kwenda katika shule zingine zisizo katika programu. Lengo ni kuharakisha maendeleo na kuleta usawa katika shule zote kwa wakati mmoja.
Naye Afisa Elimu msingi katika halmashauri ya Mji Ifakara ndugu Sylevester aliwashukuru viongozi wa CIC na CDO kwa kuleta programu hiyo katika shule za wilaya hiyo na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano unaohitajika. “Nimejionea tofauti ya mwonekano kati ya darasa la awali, darasa la kwanza na la pili. Ningependa kuona madarasa hayo yakifana ili mtoto anapoingia darasa la kwanza asione tofauti kubwa kati ya alikotoka na aendako” alisema ndugu Sylvester.
Kwa upande wake Mwl Wilson Anatory aliyemuwakilisha Afisa Elimu Mkoa wa Morogoro Eng. Joyce Baravuga alitoa shukurani kwa mashirika ya CIC na CDO kwa kuuchagua mkoa wa Morogoro katika ya mikoa miwili Tanzania iliyo katika programu yao. Zaidi aliwapongeza kwa kuamua kufanya kazi katika vijiji vilivyopo katika wilaya za pembezoni mwa mkoa wa Morogoro badala ya huduma zote kupatikana maeneo ya mjini. Zaidi aliwahakikishia ushirikiano katika kufanikisha programu hiyo na kuwaomba kupanua wigo ili kuzishirikisha shule nyingi zaidi za Mkoa mzima wa Morogoro. Aliwataka kuitumia ‘youtube channel’ ya ETETA TV inayomilikiwa na Idara ya Elimu Mkoa wa Morogoro katika kutekeleza programu yao ili taarifa ziweze kuwafikia haraka wananchi wote.
Mjadala ulihitimishwa kwamba, baada ya tathmini hiyo yatapangwa mafunzo mengine ndani ya mwaka huu 2021 kwaajili ya walimu wa madarasa ya awali, walimu wakuu wa shule, wazazi na kamati za shule, maafisa elimu kata na wengineo ili kuzifikia shule nyingi zaidi ambazo bado hazijanufaika na programu hii. Hongereni sana CIC na CDO, karibuni tena Morogoro ili kazi iendelee.
Idara ya Elimu Mkoa wa Morogoro
©2021