ETETA | Home juu

Magereza Yarejesha Eneo kwa Wananchi Ifakara, RC akumbusha wazazi kuwapeleka watoto shule

Serikali kupitia Jeshi la Magereza Nchini imerejesha eneo la hekari 50 kwa wananchi wa kitongoji cha Nakafuru, kijiji cha Milola kata ya Kibaoni Halmashauri ya Mji wa Ifakara lililokuwa linamilikiwa na Jeshi hilo tangu mwaka 2010 kwa lengo la kujenga Magereza ya Mahabusu.

Akifikisha Ujumbe wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli wa kurejesha eneo hilo kwa wananchi, Kamishna Mkuu wa Jeshi la Magereza Nchini Faustin Kasike amesema eneo hilo kwa sasa ni la wananchi wa kijiji hicho wanaostahili na kuagiza pasitokee mgogoro wowote.

“Natambua sote tunafahamu kwamba Jeshi la Magereza lilkuwa na mpango wa kujenga Magereza katika Wilaya hii ya Kilombero katika Eneo hili la Milola, lakini sasa Mhe. Rais ameamua kurejesha eneo hili kwenu wananchi ili mliendeleze”, alisema Kasike.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Sanare pamoja na kuishukuru Serikali ya awamu ya tano kwa kuwajali wananchi wake, ameitaka Halmashauri hiyo kuhakikisha wananchi walionyang’anywa maeneo yao ndio wapatiwe haki yao.

Aidha Sanare hakusita kuwakumbusha wazazi ambao watoto wao wamechaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka 2020 kuhakikisha wanawapeleka shuleni pindi shule zinapofunguliwa kwa kuwa elimu ni haki yao ya msingi.

Naye Mkuu wa Wilaya hiyo James Ihunyo amesema Halmashauri yake itahakikisha inasimamia vyema maeneo hayo ili wananchi wenye haki warejeshewe haki yao.

Hata hivyo wananchi wa Halmashauri hiyo pamoja na kuishukuru Serikali kwa kuwarejeshea eneo lao, wameiomba kuangalia uwezekano wa kuwalipa fidia kwani hawakuwa wakifanya shughuri yoyote kwa karibu kipindi cha miaka tisa huku baadhi ya nyumba zilizojengwa awali zikiharibika.

Kwa kipindi cha karibu miaka tisa wananchi wa eneo hilo wamekuwa wakidai kurejeshewa eneo hilo ambalo awali walikuwa wakilitumia kwa shughuli za makazi kabla ya Jeshi la Magereza kulichukua kwa lengo la kujenga Magereza.

                                                                           MWISHO

Wahisani

  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani