ETETA | Home juu

IDARA YA ELIMU MANISPAA YA MOROGORO YAWA KIVUTIO MAONESHO YA NANENANE 2020

Pichani ni N/Waziri wa Viwanda na Biashara Eng. Stella Manyanya (Wa pili kutoka kulia); anayefuata kulia kwake ni Mwenyeji wake Mkurugezi wa Manispaa ya Morogoro Mhe. Sheilla Lukuba wakisikiliza maelezo toka Idara ya Elimu Msingi na Sekondari.

Wao wanajiita kiwanda cha kutengeneza rasilimali watu ya nchi, hawa ni Idara ya Elimu Msingi na Sekondari Manispaa ya Morogoro. Wanaendelea kujinadi kuwa, bila wao hakutakuwa na maonesho ya nanenane kwasababu ndiyo wanaotengeneza wahitimu mahili katika fani mbambali ikiwemo wakulima na wafugaji wanaosherehekewa kupitia maonesho hayo. Mimi ni nani hadi niwabishie sasa?

Banda lao linalopatikana katika viwanja vya nanenane jengo la halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, limesheheni zana mbalimbali zinazotumika katika ufundishaji wao. Zana hizi zinabuniwa na kutengenezwa katika vituo vya walimu (Teachers’ Resource Center) na kusambazwa shuleni kwaajili ya kumrahisishia kazi mwalimu. Ukifika pale unaweza ukataka kuuziwa mfano wa kompyuta ukidhani ni  kompyuta halisi. 

Vilevile, wanatoa elimu juu ya mifumo ya kusajili au kuhamisha  mwanafunzi kutoka shule moja kwenda shule nyingine katika mkoa wowote Tanzania kwa njia ya mtandao bila kusafiri. Hii ni mifumo ya ‘Prem’ kwa shule za msingi  na ‘Prems’ kwa shule za sekondari,  inayomsaidia mzazi au mlezi kuokoa rasilimali muda na pesa za safari na hivyo kujiingiza katika shughuli zingine za uzalishaji ikiwemo kilimo.

Kitu cha pekee sana  katika idara hii, utakutana na ETETA TV (Elimu kwa Tehama Tanzania Televisheni). Kama Idara wameamua kutafsiri mitaala ya shule za msingi na sekondari inayotambuliwa na Taasisi ya Elimu Tanzania kutoka katika vitabu kwenda katika video.  Kwa kutumia walimu mahili, Mada za masomo ya msingi na sekondari zimerekodiwa katika video na kuwekwa katika mtandao wa youtube channel ya ETETA TV.  Hii ni hatua muhimu sana hasa pale inapojitokeza changamoto ya upungufu wa walimu.

Hapo mwanafunzi au mtu yeyote anaweza kujifunza akiwa popote Tanzania  au hata nje ya nchi kupitia simu yake au Kompyuta. Watu wenye ‘Flash disk’ wanaofika kwenye banda hilo la Idara ya Elimu Msingi na Sekondari Manispaa ya Morogoro wamekuwa wakipatiwa video hizo bila gharama yoyote.

Mmoja wa wahudumu katika idara hiyo alieleza kuwa, video hizo ziliweza kuwa msaada sana hasa wakati ule wa likizo ya COVID-19 ambapo wanafunzi waliendelea kujisomea kwa njia ya mtandao wakiwa nyumbani.

Linapokuja suala la watahiniwa binafsi (Private candidates), video hizo zitaendelea kuwa msaada kwao na kuwasaidia kujifunza kwa muda wowote wanaohitaji bila. 

Ikumbukwe kuwa ETETA TV, imekuja kama sehemu ya utekelezaji wa sera ya elimu kwa Tehama inayotekelezwa mkoani Morogoro tangu mwaka 2018. Kuifahamu zaidi sera hiyo, tembelea tovuti www.eteta.ac.tz . Ukweli ni kwamba, ubunifu huu hautainufaisha Morogoro pekee bali nchi nzima ya Tanzania.

Maonesho ya nanenane kanda ya mashariki yanaendelea Mkoani Morogoro yakihusisha mikoa minne ya Morogoro, Pwani, Dar es Salaam na Tanga. Kauli mbiu ya mwaka huu ni kuwa; “Kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Chagua viongozi bora 2020”.

Imeandaliwa na; Wilson Anatory

ETETA TV - MOROGORO

Wahisani

  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani