ETETA | Home juu

HIVI NDIVYO TEHAMA INAVYOENDA KUMALIZA CHANGAMOTO YA UPUNGUFU WA WALIMU MKOANI MOROGORO

(Pichani ni Afisa Elimu Taaluma Tehama ndugu Enock Juliely akitoa maelezo kuhusu upatikanaji wa video za masomo ETETA TV wakati wa maonesho ya nanenane 2020 ya kanda ya mashariki yanayofanyika Mkoani Morogoro)

Siku chache zilizopita nilibahatika kumsikiliza Afisa elimu taaluma Tehama mkoa wa Morogoro ndugu. Enock Juliely, akitoa maelezo ya mkakati wa kumaliza changamoto ya upungufu wa walimu kwa kutumia TEHAMA. Katika maelezo yake alisema kuwa; kupitia mpango unaoendelea wa kurekodi na kurusha vipindi vya masomo kwa njia ya mtandao (ETETA TV), watahakikisha wanarekodi video za mada zote za masomo ya shule za msingi na sekondari (kidato cha 1 hadi 4) na kuzihifadhi katika mifumo mbalimbali ikiwemo CD. Kila mada itarekodiwa katika nadharia na vitendo kuanzia mwanzo hadi mwisho kwa masomo yote.

Video hizo zitaendelea kusaidia pale itakapotokea shule yoyote mkoani Morogoro kuwa na upungufu au kukosa mwalimu wa somo husika. “Tukishakuwa na video hizi, ni rahisi kwa shule husika kununua screen ya kuonyeshea masomo haya kwa wanafunzi chini ya usimamizi mdogo wa mwalimu. Tutarekodi vipindi vyote vya nadharia na vitendo” Alisema Mr. Enock. Njia hii italeta nafuu hasa kwa baadhi ya walimu wanaolazimika kufundisha mikondo mingi ya madarasa.

Jambo hili linakuja wakati mwafaka ambapo serikali imejitahidi sana kusambaza umeme vijijini chini ya Wakala wa nishati vijijini (REA). Moja ya matumizi ya umeme huo, ni kurahisisha shughuli za ufundishaji na ujifunzaji mashuleni kwa njia ya TEHAMA.

Pia, mpango huo unawiana na sera ya Idara ya Elimu Mkoa ya “Elimu kwa Tehama Tanzania, (ETETA)” yenye lengo la kuufanya mkoa wa Morogoro kuwa wa kidijitali ifikapo mwaka 2022. Tayari video nyingi za masomo ya shule za msingi na sekondari zimeshaanza kupatikana katika mtandao wa youtube kwenye channel ya ETETA TV.

Imeandaliwa na;

Wilson Anatory

ETETA TV - MOROGORO

Wahisani

  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani