ETETA | Home juu

MOROGORO TUNAYE ‘REO’ ANAYEITENDEA HAKI TEHAMA

(Pichani ni Afisa Elimu Mkoa wa Morogoro (kulia) akiwa na Mkurugenzi wa taasisi ya APPS AND GIRLS katika mafunzo ya kuwaongezea ujuzi walimu wa Manispaa ya Morogoro juu ya Elimu Mtandao iliyofanyika katika shule ya sekondari Morogoro mwezi Juni, 2020)

Sehemu ya 1

Ili kutohukumiwa na wale waliosema kuwa 'Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni' naomba niyaseme haya juu ya REO wetu Eng. Joyce Baravuga na Idaya yake nzima ya Elimu Mkoa wa Morogoro ili kuwatia moyo katika utendaji wao.

Nikiwa kama mwalimu na mdau wa Elimu, kwa macho, masikio na akili yangu nimeona, nimesikia na kuamini kuwa Morogoro tunaye REO anayeitendea haki TEHAMA. Ninayo mifano kadhaa ya kulithibitisha hili na ndiyo lengo kuu ya makala hii.

Ni chini ya mwaka mmoja tangu nimemfahamu kiongozi huyo, lakini kwa muda huo mfupi nimefurahishwa sana kwa jinsi anavyoitendea haki TEHAMA ndani ya mkoa wake hasa katika sekta ya Elimu. Chini ya REO Baravuga, Idara ya Elimu Mkoa wa morogoro inaongozwa na falsafa bora kabisa ya 'Elimu kwa TEHAMA Tanzania'. Ikumbukwe kuwa falsafa ni msimamo anaouamini mtu unaomwongoza katika kila hatua ya maisha yako. Bila shaka ushindi wake katika kuitendea haki TEHAMA umejificha katika falsafa hiyo.

Mnamo Septemba 2019, nilipata fursa ya kuratibu mafunzo ya TEHAMA kwa walimu wa mkoa wa Morogoro yaliyotolewa kwa ushirikiano wa taasisi binafsi na za serikali na kufanyika pale Chuo kikuu cha Jordan - Morogoro.

REO Eng. Baravuga alikuja kushiriki mafunzo hayo na alikaa viti vya kawaida kama washiriki wengine walimu. Kama asingepewa nafasi ya kuzungumza kwa ufupi inawezekana kabisa baadhi ya walimu wasingetambua kuwa mmoja wa washiriki/wanafunzi wa TEHAMA alikuwa ni REO wetu Eng. Baravuga. Hakujitofautisha kabisa na walimu wengine.

Wala hakujali umri au nafasi za wakufunzi waliokuwa wanatoa mafunzo hayo yaliyolenga kujifunza ‘Scratch Program for teachers’. Alikaa na kujifunza mwanzo hadi mwisho wa program.

Mwaka jana 2019 nilipotoa kitabu changu cha MHITIMU ANAYEHITAJIKA KTK SOKO LA AJIRA, kabla ya kukipokea akiwa ofisini kwake aliniuliza swali; 'Kitabu chako kimegusia suala la TEHAMA?' Nilimhakikishia kuwa TEHAMA ni sehemu ya Mhitimu anayehitajika katika soko la ajira tulilonalo, haikuachwa nyuma kwenye kitabu hicho. Kisha nikamsomea paragraph moja tu (Uk 24) isemayo kuwa;

'Kosa kubwa tunaloweza kufanya leo ni kumwacha mwanafunzi ahitimu shule ya msingi, sekondari au chuo bila kuwa na ujuzi wa matumizi ya TEHAMA. Katika dunia ya sasa kila mtu anatakiwa kuwa na angalau ujuzi wa wastani katika matumizi ya kawaida ya Kompyuta na TEHAMA kwa ujumla. Ni ajabu kwa mhitimu wa leo kukosa ujuzi wa kompyuta katika shughuli za kawaida za kila siku kama vile kuchapa taarifa mbalimbali, kutumia mtandao kutuma na kupokea barua pepe pamoja na kuperuzi taarifa mbalimbali'. Hapo alichukua nakala yake tukaendelea na mambo mengine.

Katika hatua nyingine, Morogoro ni moja ya mikoa michache Tanzania ambayo shule zake zinanufaika na mpango wa ADSI ( African Digital Schools Initiative). Huu ni mpango unaolenga kueneza matumizi ya TEHAMA katika shule za Afrika ikiwemo Tanzania. Ni mpango unaolenga kuhakikisha kuwa teknolojia inakuwa sehemu ya maisha ya kila siku ya walimu na wanafunzi ndani na nje ya shuke na hivyo kurahisiha ujifunzaji na ufundishaji.

Mwishoni mwa mwaka jana 2019 nilipata nafasi ya kuhudhuria tukio lililoandaliwa na ADSI, la kukabidhi vyeti kwa walimu wa Mkoa wa Morogoro waliofuzu sehemu ya mafunzo ya TEHAMA. Mwakilishi toka Idara ya Elimu Mkoa wa Morogoro alieleza kuwa, TEHAMA ni kipaumbele sana katika mkoa wa Morogoro. Kila mwalimu anayeshiriki mafunzo hayo ni lazima ayafanye kwa nguvu zote bila mzaha.

Inaendelea sehemu ya 2

Imeandaliwa na;

Wilson Anatory

ETETA TV - MOROGORO

Wahisani

  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani