ETETA | Home juu

WAZIRI KABUDI AZINDUA MAONESHO YA NANENANE MKOANI MOROGORO

Ni maonesho ya 27 ya wakulima na wafugaji  maarufu kama Nanenane yaliyozinduliwa tarehe 1 agosti 2020 na mgeni rasmi Waziri wa Mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa Prof. Paramagamba Kabudi. Maonesho hayo ya kanda ya mashariki yameshirikisha mikoa minne ikiwemo Morogoro, Pwani, Dar es Salaam na Tanga.

Baada ya kutembelea mabanda ya maonesho na kujionea mbinu na faida mbalimbali zitokanazo na shughuli za kilimo na ufugaji Prof. Kabudi ametoa wito kwa wananchi kujenga tabia ya kutembelea maonesho ya Nanenane ili kupata elimu mpya ya kilimo, ufugaji na uvuvi.

Akimshukuru Mungu kwa kutuepusha na janga la Corona, ameonesha kutambua thamani ya mimea tiba ambayo wananchi wengi wamekuwa wakiitumia kama tiba asili ya kujikinga na virusi vya Corona (COVID-19). Amesisitiza wananchi kutoisahau mimea tiba wanapopanda mazao mengine ya chakula. “Niwahakikishe kuwa, ndani ya miaka mitano ijayo, miti dawa na mimea dawa itakuwa biashara kubwa, sio tanzania tu bali duniani kote” Alisema Prof. Kabudi.

Aidha ameikumbusha mikoa yote ya kanda ya mashariki jukumu kubwa walilonalo la kuhakikisha Tanzania inapaa kiuchumi kutokana na shughuli za kilimo katika maeneo hayo. Akirejea nia ya Hayati Mwalimu Nyererea lipoamua kujenga viwanda vingi mkoani Morogoro alieleza kuwa, Morogoro ni mkoa wenye ardhi na hali ya hewa nzuri inayowezesha kilimo cha mazao ya aina karibia zote na kilimo hufanyika kwa zaidi ya msimu mmoja kwa mwaka.

Pia, Morogoro ni mkoa uliokuwa na nishati ya umeme wa kutosha kutokana na mabwawa makubwa ya kuzalishia umeme yaliyokuwepo.  Umeme huo ndiyo uliokuwa ukitegemewa kuendeshea viwanda vilivyojengwa kwaajili ya usindikaji wa mazao. Zaidi ni kuwa, Mkoa wa Morogoro uko karibu na bandari mbili kubwa za Dar es Salaam na Tanga kwaajili ya kusafirisha mazao ya kilimo kwenda nchi za nje na hivyo kurahisisha biashara.

Kwa msingi huo, Prof. Kabudi amewakumbusha viongozi na wananchi wa mikoa yote ya mashariki kutambua kuwa bado wanalo jukumu hilo la kuhakikisha kuwa wanakuwa kiungo muhimu katika kuipaisha nchi yetu kiuchumi. “Morogoro na kanda ya mashariki ndiyo injini yenye jukumu kubwa la kuifanya nchi yetu ipae kiuchumi” Alisema Prof. Kabudi.

Amesisitiza matumizi ya njia bora za kilimo kuanzia kwenye ulimaji, uvunaji, utunzaji na usindikaji wa mazo ya kilimo. Hii ni pamoja na kuongeza ubora na thamani ya mazao ili wakulima waweze kunufaika vyema na kazi zao za kilimo, uvuvi na ufugaji.  

Katika hatua nyingine, Prof Kabudi ameahidi kupeleka ombi lililotolewa la maonesho ya Kanda ya mashariki kuwa ya kitaifa hapo mwakani 2021. Amewashukuru na kuwapongeza sana wakuu wa mikoa yote ya Morogoro, Pwani, Dar es Salaam na Tanga kwa kusimamia vyema maandalizi yote ya maonesho hayo ya kanda ya mashariki mwaka 2020. Pia amewapongeza makatibu tawala wa mikoa hiyo kwa usimamizi mzuri wa maonesho hayo, na kuwatakiwa kila la kheri wananchi wote katika kushirki maonesho hayo. Maonesho ya 27 ya ya wakulima na wafugaji nanenane yatafikia kilele chake tarehe 8 agosti 2020.

Imeandaliwa na; Wilson Anatory

ETETA TV - MOROGORO  

Wahisani

  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani