ETETA | Home juu

AFISA ELIMU MOROGORO AFANYA MAKUBWA KWA WANAFUNZI KILAKALA SEKONDARI WALIPOTEMBELEA IDARA YA ELIMU MAONESHO YA NANENANE

(Pichani ni Afisa Elimu Sekondari Manispaa ya Morogoro Dkt. Janeth Balongo (Kushoto) akicheza mchezo wa Chemshabongo na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kilakala Walipotembelea Idara ya Elimu katika maonesho ya nane nane mkoani Morogoro)

Moja ya shule zilizojizolea umaarufu mkoani Morogoro na Tanzania nzima ni shule ya sekondari Kilakala iliyopo katika halmashauri ya manispaa ya Morogoro.  Hii ni shule ya serikali maalumu kwa watoto wenye ufaulu mkubwa. Kwa kifupi ni shule ya wanafunzi wenye vipaji maalumu.

Leo tarehe 5 agosti 2020, wanafunzi hao wa shule ya sekondari Kilakala waliweza kutembelea banda la Idara ya Elimu halmashauri ya Manispaa Morogoro inayoshiriki katika maonesho ya nanenane yanayoendelea mkoani Morogoro. Tofauti na wanafunzi wengi tuliowazoea, wanafunzi wengi wa Kilakala sekondari walionekana kuwa na daftari ndogo (note book) kwaajili ya kuandika kile walichokuwa wakijifunza kwenye mabanda tofauti tofauti ya maonesho. Hii ndiyo namna halisi ya kujifunza, hongereni sana walimu Kilakala sekondari kwa kuwalea hivyo watoto wetu.

Sina hakika kama inatokana na umaalumu wa shule yao, lakini wanafunzi hao walibahatika kumkuta Afisa Elimu sekondari Manispaa ya Morogoro Dkt. Janeth Balongo naye akiwa amekuja kukagua maendeleo ya maonesho katika banda hilo. Kitu kikubwa alichokifanya Afisa huyo, aliamua kuacha mambo yake yote na kushirikiana na walimu wengine walioandaliwa kufafanua mambo mbalimbali yanayofanywa na Idara ya Elimu manispaa ya Morogoro.

Pamoja na mambo mengine, Dkt. Balongo alishiriki kucheza michezo ya chemsha bongo pamoja na wanafunzi hao. Wanafunzi walifurahi sana kwa mapokezi na ukarimu walioupata katika banda hilo ambalo ndilo linalosimamia mustakabali wa masomo yao shuleni.   

Jambo hili liliwakonga nyoyo hata walimu waliokuwa wameambatana na wanafunzi hao kwa kumwona kiongozi huyo akichukua nafasi ya kufundisha wanafunzi kazi ambayo imezoeleka kufanywa na walimu. “Naona wanafunzi wetu wamepata bahati ya kujifunza moja kwa moja kutoka kwa Afisa Elimu” alisema Mwalimu Abel Mkangwa. Naye Mwalimu Patrick Mwaijonga alisema kuwa, “Banda hili tutaendelea kuwa wageni wenu kwa siku tatu mfululizo. Kutokana na wingi wa wanafunzi tumeamua kuwagawa katika makundi matatu, kesho tutakuja hapa na kundi jingine”.

Banda la Idara ya Elimu (Msingi na Sekondari) linapatikana katika jengo la maonesho la halmashauri ya manispaa ya Morogoro. Maonesho ya nanenane kanda ya mashariki yanahusisha mikoa ya Morogoro, Pwani, Dar es Salaam na Tanga yakiwa na kauli mbiu; “Kwa maendeleo ya kilimo, mifugo na uvuvi chagua viongozi bora 2020.

Imeandaliwa na;

Wilson Anatory

ETETA TV - MOROGORO

Wahisani

  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani
  • Wahisani