PROGRAMU YA ‘WATOTO WETU TUNU YETU’ KUWANUFAISHA WATOTO WENGI ZAIDI MKOANI MOROGORO
(Pichani
ni viongozi kutoka mashirika yanayojihusisha na watoto ya CIC na CDO pamoja na
viongozi mbalimbali wa Elimu Mkoani Morogoro walipotembelea wanafunzi wa darasa
la awali katika shule ya Msingi Ngai iliyoko katika kata ya Mchombe Wilayani
Mlimba Mkoani Morogoro tarehe 24/5/2021)
Moja ya kitu
tunachojivunia hapa kwetu Morogoro ni uwepo wa taasisi (NGOs), Mashirika na
watu binafsi wanaofanya kazi kwa kushirikiana na serikali katika kuwahudumia
watanzania. Unakumbuka jinsi taasisi na wadau wa elimu walivyogombania fursa ya
kumwendeleza mtoto Charles Mathias aliyegundulika kuwa na kipaji katika
hisabati akiwa darasa la awali huko halmashauri ya Morogoro vijijini?
Leo tutawazungumzia wadau
wetu wengine wa elimu ambao kwa nafasi yao wameweza kufanya makubwa sana katika
kuunga juhudi za serikali za kuwahudumia wananchi hasa katika utoaji wa elimu
ya awali. Ni nani hao na wamefanya nini kuwanufaisha watoto wetu? Majibu yote
ni katika aya zifuatazo.
Mwaka 2018, Shirika la
kimataifa la ‘Children in Crossfire (CIC)’ lenye ofisi zake jijini Dar es
Salaam kwa kushirikiana na taasisi nyingine ya wazawa ya ‘Children Development
Organization, (CDO)’ ya Morogoro waliomba kushirikiana na serikali katika kutoa
maandalizi mazuri ya watoto wadogo kwaajili ya kujiunga na darasa la kwanza.
Mashirika yote hayo mawili yana malengo yanayofanana ya kusimamia malezi na
maendeleo mazuri ya watoto wadogo kati ya miaka 3 hadi 6. CIC na CDO wanaamini
kwamba ili mtoto afanikiwe katika taaluma za madarasa ya juu ni lazima ajengewe
msingi bora wa malezi kupitia elimu ya awali.
Mashirika hayo hulenga
zaidi maeneo ya vijijini ambako watoto wengi hukosa fursa ya elimu ya awali na
kupitia changamoto nyingi zinazoathiri makuzi na maendeleo yao. Katika kutimiza
wajibu wao, CIC na CDO hufanya mambo yafuatayo;
i)
Kuhamasisha uanzishaji wa vituo vya watoto
(day care centers) vya kijamii vyenye gharama nafuu kwa mzazi kulipia.
ii)
Kutoa mafunzo ya utoaji wa elimu ya awali
kwa walimu, wakuu wa shule, maafisa elimu wilaya na kata, viongozi wa kijiji,
wazazi nk.
iii)
Kufadhiri vifaa vya kufundishia na
kujifunzia kwa watoto wadogo kama vile makabati ya kutunzia vifaa, penseli,
vitabu, michoro nk.
iv)
Kusimamia masuala ya lishe na usalama wa
mtoto.
v)
Kuboresha miundombinu ya darasa la awali.
vi)
Kulea vituo vilivyoanzishwa na kutengeneza
mifumo ya kuweza kujiendesha hata baada ya wao kuondoka.
vii)
Kufanya tathmini na kushauri serikali juu
ya mabadiliko au maboresho ya sera zinazosimamia watoto yanayohitajika
kutegemeana na mahitaji ya wakati uliopo.
Kwa sasa CIC na CDO
wanafanya kazi katika mikoa miwili pekee ambayo ni Dodoma na Morogoro. Kwa hapa kwetu Morogoro wamekuwa wakifanya
kazi katika wilaya za Mvomero, Ifakara na Mlimba tangu mwaka 2018 ambapo mradi
huo unatarajiwa kukamilika mwaka 2022.
Kuanzia tarehe 24 hadi
27/5/ 2021, viongozi wa CIC na CDO walikuwa wakifanya tathmini ya mafanikio
yaliyopatikana katika programu yao kwa muda wote tangu walipoanza. Miongoni mwa
viongozi hao alikuwa ndugu Heri Ayubu ambaye ni Msimamizi Mkuu wa Mipango na
uendeshaji pamoja na Frank Samson kutoka shirika la CIC. Wengine ni ndugu Marsel
Salema na Joseph Machira ambao ni viongozi kutoka CDO. Viongozi hao
waliambatana na Mwl. Wilson Anatory ambaye ni Afisa kutoka Idara ya Elimu Mkoa
aliyemuwakilisa Afisa Elimu Mkoa wa Morogoro Eng. Joyce M. Baravuga.
Zoezi hili lilifanyika
kwa kutembelea Wilaya za Mlimba na Ifakara na kukagua vituo vilivyokuwa
vikinufaika na programu hiyo pamoja na vile visivyonufaika ili kupata
ulinganifu. Pia, walizungumza na Maafisa elimu Wilaya na Kata, Maafisa wa
ustawi wa jamii, kamati za shule, wazazi, walimu wakuu wa shule na walimu wa
darasa la awali katika shule husika.
Shule zilizotembelewa ni
pamoja na Shule ya Msingi Ngai iliyopo katika kata ya Mchombe na shule ya
msingi Ngajengwa iliyopo katika kata ya Igima zote Wilayani Mlimba. Pia walitembelea kituo cha
watoto wadogo (day care school) cha Mt.
Yohana kilicho chini ya kanisa katoliki Mlimba. Shule nyingine ni Shule ya
msingi Darajani iliyopo katika kata ya Mwaya Wilayani Ifakara pamoja na kituo
cha watoto cha Upendo kilichopo katika wilaya hiyo.
Kwa ujumla wadau wote
hapo juu walionesha kufurahia programu hiyo kwakuwa imesaidia watoto wengi kuwa
katika mikono salama ya walimu badala ya kuachwa mitaani ambako hakuna uhakika
wa kesho yao.
Wazazi wengi wamehamasika
kuchangia maendeleo ya watoto wao na hata kushiriki shughuli ndogondogo za
kuandaa zana za kufundishia watoto kwa kushirikiana na mwalimu wa darasa la
awali. Kamati za shule zimeweza kujitengenezea mpango kazi unaowaongoza katika
mipango yao ya mwaka ya uendelezaji wa shule na watoto.
Walimu wa madarasa ya
awali kwa kushirikiana na walimu wakuu wa shule wameweza kuboresha mandhari ya
madarasa ya awali kuwa na muonekano unaoshauriwa kitaalamu kwa kupanga sehemu
kuu za darasa kama vile sehemu ya kusomea vitabu, sehemu ya kuandikia, sehemu
ya kucheza, sehemu ya kufanyia sanaa nk.
Pia, madarasa yamepambwa vizuri kwa picha na maandishi ya kujifunzia watoto
kama inavyoshauriwa kitaalamu.
Katika majumuisho ya
ziara hiyo yaliyomshirikisha Afisa Elimu Msingi halmashauri ya Mji Ifakara
ndugu Sylvester Kalagile pamoja na Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Darajani,
viongozi wa CIC na CDO walishukuru sana kwa ushirikiano walioupata tangu siku
ya kwanza hadi ya mwisho katika ziara yao ya kufanya tathmini. Walionesha kufurahishwa
na jinsi wazazi walivyoitikia uhamasishaji wao na kuwezesha shule kujisimamia
zenyewe.
Sambamba na hilo, walitoa
wito kwa viongozi wa elimu wakiwemo Maafisa elimu Wilaya na kata, walimu wakuu
wa shule na wadau wengine kujifunza na kuhamisha mambo mazuri yaliyo katika
shule zilizonufaika na programu kwenda katika shule zingine zisizo katika
programu. Lengo ni kuharakisha maendeleo
na kuleta usawa katika shule zote kwa wakati mmoja.
Naye Afisa Elimu msingi
katika halmashauri ya Mji Ifakara ndugu Sylevester aliwashukuru viongozi wa CIC
na CDO kwa kuleta programu hiyo katika shule za wilaya hiyo na kuahidi
kuendelea kutoa ushirikiano unaohitajika. “Nimejionea tofauti ya mwonekano kati
ya darasa la awali, darasa la kwanza na la pili. Ningependa kuona madarasa hayo
yakifana ili mtoto anapoingia darasa la kwanza asione tofauti kubwa kati ya
alikotoka na aendako” alisema ndugu Sylvester.
Kwa upande wake Mwl
Wilson Anatory aliyemuwakilisha Afisa Elimu Mkoa wa Morogoro Eng. Joyce
Baravuga alitoa shukurani kwa mashirika ya CIC na CDO kwa kuuchagua mkoa wa
Morogoro katika ya mikoa miwili Tanzania iliyo katika programu yao. Zaidi
aliwapongeza kwa kuamua kufanya kazi katika vijiji vilivyopo katika wilaya za
pembezoni mwa mkoa wa Morogoro badala ya huduma zote kupatikana maeneo ya
mjini. Zaidi aliwahakikishia ushirikiano katika kufanikisha programu hiyo na
kuwaomba kupanua wigo ili kuzishirikisha shule nyingi zaidi za Mkoa mzima wa
Morogoro. Aliwataka kuitumia ‘youtube channel’ ya ETETA TV inayomilikiwa na Idara
ya Elimu Mkoa wa Morogoro katika kutekeleza programu yao ili taarifa ziweze
kuwafikia haraka wananchi wote.
Mjadala ulihitimishwa
kwamba, baada ya tathmini hiyo yatapangwa mafunzo mengine ndani ya mwaka huu
2021 kwaajili ya walimu wa madarasa ya awali, walimu wakuu wa shule, wazazi na
kamati za shule, maafisa elimu kata na wengineo ili kuzifikia shule nyingi
zaidi ambazo bado hazijanufaika na programu hii. Hongereni sana CIC na CDO,
karibuni tena Morogoro ili kazi iendelee.
Idara ya Elimu Mkoa wa Morogoro
©2021